29.4 C
New York

Saudia ilivyobaki njiapanda vita vya Iran

Published:

RIYADH, Saudi Arabia

SAUDI Arabia imebaki njiapanda. Tangu Marekani na Israel zilipoungana kuishambulia Iran, Saudia ilijiweka mbali na mgogoro huo. Haikutaka kujihusisha wala kuhusishwa.

Hata hivyo, ukaribu wake na Marekani umeiponza na kujikuta ikishambuliwa na Iran, pamoja na washirika wake kutoka Ukanda wa Mashariki ya Kati.

Mapema wiki hii, Saudia iliungana na Marekani kufanya mashambulizi dhidi ya vikundi vya kigaidi vya Iraq vinavyoiunga mkono Iran.

Hatua hiyo ya kujibu ilikuja baada ya Saudia kushambuliwa na Iran na vikundi vya Houthis (Yemen), Popular Mobilisation Forces (PMF) na Hezbollah (Lebanon).

Taarifa zinaeleza kuwa PMF imeshafanya mashambulizi ya ndege zisizo na rubani (drones) zaidi ya 30 nchini Saudia.

Hivyo, wakati huu Saudia ikijaribu kujibu, bado nchi hiyo imebaki njiapanda, kwamba iendelee kushambulia au itafute namna ya kujitoa kwenye vita?

Saudia inafahamu kuwa vita ni gharama. Kujiingiza katika mgogoro huo unaoihusu Marekani na Iran kutaharibu miundombinu yake, hivyo kuathiri kwa kiasi kikubwa mipango mingi ya maendeleo.

Ikumbukwe, Saudia chini ya Mwanamfalme Mohammed Bin Salman inatekeleza Dira yake ya Mwaka 2030 inayolenga kuboresha sekta ya viwanda na kuifanya nchi hiyo kuondokana na utegemezi wa mapato yatokanayo na nishati ya mafuta.

Kwa kujenga viwanda vingi na vya kisasa, Saudia imelenga kupungua changamoto kubwa ya uhaba wa ajira, hasa kwa vijana wake wanaohitimu elimu ya juu.

Sambamba na hilo, Dira ya 2030 inasisitiza mazingira rafiki kwa uwekezaji wa nje, ikiwamo ujenzi wa vituo vya takwimu. Hayo yanawezekana vipi endapo nchi itakuwa kwenye vita?

Vilevile, Saudia inajifunza kutoka kwa Israel, ambayo licha ya urafiki wake mkubwa na wa kihistoria na Marekani, haijaingiza miguu yote katika vita dhidi ya Iran.

Related articles

Recent articles