Na mwandishi wetu, Gazetini
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, ameibuka mshindi tena dhidi ya Jamhuri katika hatua nyingine ya kesi ya uhaini inayomkabili, baada ya Mahakama ya Rufani kutupilia mbali maombi ya upande wa mashtaka yaliyolenga kuruhusiwa kuwasilisha ushahidi wa nyongeza.
Pamoja na ushindi huo, Mahakama ya Rufani imekataa ombi la Lissu lililotaka Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) aagizwe kumlipa fidia kwa kile alichodai ni ucheleweshaji wa usikilizwaji wa kesi ya msingi.
Jamhuri iliwasilisha maombi hayo ya mapitio Februari 24, 2026, ikipinga uamuzi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam, ambao ulikataa ombi lake la kuruhusiwa kuwasilisha ushahidi wa nyongeza katika kesi ya uhaini inayomkabili Lissu.
Shauri hilo la mapitio namba 7203216/2026 lilisikilizwa Julai 3, 2026 mbele ya jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani likiongozwa na Jaji Augustine Mwarija, akishirikiana na Majaji Zainabu Muruke na Amour Khamis.
Katika uamuzi uliotolewa leo, Alhamisi Julai 30, 2026, Mahakama ya Rufani iliridhia msimamo wa Mahakama Kuu pamoja na hoja zilizowasilishwa na Lissu, na hivyo kuyatupilia mbali maombi ya Jamhuri.


