28 C
New York

Macho yote sasa WAFCON 2026

Published:

CAIRO, Misri

BAADA ya kumalizika kwa fainali za Kombe la Dunia, sasa macho na masikio ya mashabiki ya wapenzi wa soka yataelekezwa katika michuano ya WAFCON 2026.

Tofauti na AFCON, WAFCON hushirikisha timu za wanawake kutoka mataifa mbalimbali na msimu huu mashindano hayo yatafanyika nchini Morocco. .

Safari hii, timu 16 zitashiriki na mashindano hayo ya Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) yanatarajiwa kuanza wikiendi hii (Julai 26, 2026).

Wakati Nigeria ikisaka kutetea taji, timu zingine zinazoaminika kuwa na ubavu wa kutwaa ubingwa ni Ghana, Zambia na Morocco.

MIJI MIWILI, VIWANJA VITANO

Katika fainali za mwaka huu, Morocco imeandaa viwanja vitano katika miji mikubwa miwili ya Rabat na Casablanca.

Uwanja mkubwa zaidi ni Moulay Rachid wa mjini Casablanca, ambao takwimu zinaonesha kuwa una uwezo wa kupokea mashabiki 25,000.

Uwanja unaofuata kwa ukubwa ni Moulay El Hassan ulioko Rabat, ukiwa na uwezo wa kupokea mashabiki 22,000.

Uwanja wa Olimpiki wa Rabat unafuata ukiwa unapokea mashabiki 21,000, kisha Larbi Zaouli (20,000) na Al Medina (18,000).

MAKUNDI

Kundi A: Morocco, Algeria, Senegal, Kenya – Kundi B: Afrika Kusini, Ivory Coast, Burkina Faso na Tanzania – Kundi C: Nigeria, Zambia, Misri.na Malawi – Kundi D: Ghana, Cameroon, Mali na Cape Verde.

RATIBA HII HAPA

Mechi za hatua ya makundi zitaanza Julai 26 hadi Agosti 6, 2026. Hatua ya robo fainali itaanza siku mbili baadaye hadi Agosti 9.

Agosti 12, 2026, zitachezwa mechi za nusu fainali, kisha ‘playoff’ itapigwa siku inayofuata, kabla ya fainali kuchezwa Agosti 16, 2026.

Katika siku ya kwanza ya mashindano, yaani Julai 26, Algeria itaivaa Senegal, huku Morocco wakipepetana na Kenya.

REKODI

Kati ya 16 zinazoshiriki, tisa zilikuwepo wakati wa fainali za msimu uliopita, kwa maana ya WAFCON 2024.

Wakati Botswana, the DRCongo na Tunisia zikikosekana safari hii, Cape Verde na Malawi zinashiriki kwa mara ya kwanza katika historia ya michuano hiyo.

Cape Verde wanaweka rekodi hiyo zikiwa ni siku chache tu tangu ilipoandika historia ya kushiriki kwa mara ya kwanza fainali za Kombe la Dunia na kutinga hatua ya 32 Bora.

TIKETI YA KOMBE LA DUNIA

Timu nne zitakazotinga nusu fainali ya WAFCON zitafuzu moja kwa moja kushiriki fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2027 zitakazofanyika nchini Brazil.

Timu zitakazoishia robo fainali zitaingia kwenye ‘playoff’ ya kusaka tiketi mbili za kwenda kuvaana na wawakilishi wa mabara mengine kuwania nafasi ya kwenda Kombe la Dunia.

Kati ya timu 16 zilizopo msimu huu wa WAFCON, nne ziliweza kushiriki fainali zilizopita za Kombe la Dunia zilizofanyika mwaka 2023. Timu hizo ni Morocco, Nigeria, Afrika Kusini, na Zambia.

HISTORIA YA UBINGWA

Nigeria inaongoza kwa kutwaa mara nyingi ubingwa wa WAFCON, ikiwa imebeba mara 10, ikifuatiwa na Guinea ya Ikweta yenye mataji mawili (2008 na 2012) na Afrika Kusini (2022).

Licha ya kutokuchukua ubingwa, Morocco, Ghana na Cameroon zimewahi kufika fainali.

NANI KUTWAA UBINGWA 2026?

Mbali na Nigeria wanaosaka taji lao la 11, Ghana nayo nayo inapewa nafasi baada ya kufuzu ikiwa na mabao saba, pia ikiwa haijaruhusu bao.

Zambia nayo ina nafasi yake, ikizingatiwa kuwa haijakosa WAFCON kwa misimu minne mfululizo. Ni kama ilivyo kwa Morocco, ambayo ilifika fainali misimu miwili iliyopita.

VITA TUZO YA MCHEZAJI BORA

Msimu uliopita (WAFCON 2024), mshambuliaji wa Nigeria, Ajibade, ndiye aliyeondoka na tuzo ya Mchezaji Bora wa mashindano hayo.

Wakati huo huo, staa wa Morocco, Ghizlane Chebbak, ndiye aliyeibuka mfungaji bora akiwa amezifumania nyavu mara tano.

Safari hii, pia yupo Kundananji wa Zambia, ambaye misimu miwili iliyopita aliweka rekodi ya kuwa mchezaji aliyesajiliwa kwa dau kubwa zaidi katika historia ya Ligi Kuu ya Wanawake nchini Marekani (NWSL).

Nyota mwingine anayewapa jeuri mashabiki wa Zambia ni straika mkongwe Banda, ambaye anatajwa kuwa miongoni mwa vipaji vikubwa kuwahi kutokea katika soka la wanawake barani Afrika.

DAU NONO

Msimu huu, bingwa wa mashindano ataondoka na kitita cha Dola za Marekani milioni 2 (zaidi ya Sh bil. 5.2 za Tanzania). Ni mara mbili ya zawadi ya msimu uliopita (2024).

Timu itakayoshika nafasi ya pili itajiondokea na kitita cha Dola 750,000 (takribani Sh bil. 2 za Tanzania), likiwa ni ongezeko la asilimia 50 ya msimu uliopita (2024).

Related articles

Recent articles