28.1 C
New York

Huyu hapa daktari anayeua wagonjwa

Published:

BERLIN, Ujerumani

MAHAKAMA nchini Ujerumani imemuhukumu kifo cha maisha gerezani daktari aliyebainika kuua wagonjwa wake 15, wakiwamo wanawake 12.

Mwanaume huyo aliyefahamika kwa jina la Johannes M. ana umri wa miaka 41 na ametajwa na Mahakama kufanya kosa hilo kuanzia Septemba 21 hadi Julai, 2024.

Aidha, Mamlaka mjini Berlin zimedai kuwa huenda hiyo ni sehemu ndogo tu ya mauaji mengi aliyowahi kufanya daktari huyo.

Hivyo, waendesha mashitaka mjini Berlin wameitisha uchunguzi wa matukio yake mengine ili kuona kama kuna uhalifu wa aina hiyo.

Mahakama imeeleza kuwa waliouawa na daktari huyo ni wagonjwa waliokuwa na umri kati ya miaka 25 na 94.

Pia, mahakama imejiridhisha kuwa wagonjwa hao walikuwa kwenye hali mbaya lakini daktari huyo alichangia vifo vyao vya mapema.

Waendesha mashitaka wameeleza kwamba aliwapa wagonjwa wake dawa zenye madhara bila ruhusa yao alipokuwa akiwatembelea nyumbani.

Julai, 2024, kabla ya kukamatwa, waendesha mashitaka walidai kuwa daktari huyo aliua wagonjwa wawili ndani ya siku moja.

Wagonjwa hao walitajwa kuwa ni mwanaume mwenye umri wa miaka 75 mkazi wa Berlin, na mwanamke (76) anayeishi Wilaya ya jirani.

Wakati huyo huo, kwa mujibu wa waendesha mashitaka, alijaribu bila mafanikio kuichoma moto nyumba ya mwanamke huyo ili kupoteza ushahidi.

Kwa mwaka mmoja wa kesi yake, daktari huyo hakuwahi kusema chochote mbele ya mahakama, hadi Mei, 2026, alipokiri kuua wagonjwa 12 waliokuwa mahututi.

Katika utetezi wake, alisema alifikia kufanya hivyo akiamini alikuwa sahihi kuwaondoshea mateso waliyokuwa wakipitia kutokana na maradhi.

“Kwa kipindi chote hicho (cha kuua wagonjwa), niliamini nilikuwa sahihi kwa kila mmoja wao,” alisema daktari huyo, kisha kuomba radhi kwa wote waliokwazika au kuumizwa na matukio yake hayo.

Kwa sasa, waendesha mashitaka wanachunguza matukio 76 ya daktari huyo ili kuona kama kuna wagonjwa wengine alioowahi kuwaua.

Vyombo vya habari vya Ujerumani vinaeleza kuwa endapo atakutwa na hatia, basi daktari huyo ataingia kwenye rekodi ya kuwa muuaji wa kimyakimya hatari zaidi kuwahi kufokea nchini humo.

Kwa upande wa familia na watu wake wa karibu, wamesema bado hawaamini kile kilichofanywa na ndugu yao huyo.

Wakati huo huo, mama wa mmoja ya wagonjwa waliouawa, amesema binti yake mwenye umri wa miaka 25 alipoteza maisha mwaka 2021. “Hakuwahi kusema anataka kufa,” amesema mama huyo.

Mbali ya kifungo cha maisha gerezani, Mahakama pia imemfungia daktari huyo kujihusisha na taaluma ya afya kwa maisha yake yote.

Related articles

Recent articles