Na Imani Nathaniel, Gazetini
Mkurugenzi Mkuu wa Halotel Tanzania, Bui Van Thang, ametembelea banda la kampuni hiyo katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba 2026), akijionea huduma mbalimbali za kisasa na suluhisho za kidijitali zinazotolewa kwa Watanzania.
Katika ziara hiyo iliyofanyika Julai 8, 2026, Bui aliambatana na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Halotel Tanzania, Tran Thi Thuy Dung, na kuongozwa na Mkurugenzi wa Biashara wa kampuni hiyo, Abdallah Salum.
Akiwa katika banda hilo, viongozi hao walipata fursa ya kuona huduma mbalimbali zinazotolewa na Halotel ikiwemo teknolojia ya intaneti ya kasi ya 5G, Halotel Fibre kwa matumizi ya majumbani, huduma za kifedha za HaloPesa pamoja na ubunifu mwingine wa kidijitali unaolenga kurahisisha maisha ya Watanzania.

Akizungumza baada ya ziara hiyo,bBui Van Thang alisema Halotel itaendelea kuwekeza katika teknolojia na ubunifu ili kuhakikisha wateja wanapata huduma zenye ubora, uhakika na zinazokwenda sambamba na kasi ya mabadiliko ya kidijitali.
Mkurugenzi huyo pia alizungumza na wafanyakazi wanaotoa huduma katika banda hilo, akiwapongeza kwa juhudi zao za kuwahudumia wananchi na kuhakikisha wageni wanaotembelea maonesho wanapata uzoefu mzuri.


Pia alikutana na baadhi ya wateja na kushiriki kuwahudumia huku akijionea namna huduma za Halotel zinavyoendelea kusaidia mawasiliano na biashara nchini.
Kwa upande wake, Meneja Masoko wa Halotel Tanzania, Aidat Lwiza, amewahimiza Watanzania kuendelea kutembelea banda la kampuni hiyo katika viwanja vya Sabasaba ili kujionea huduma mbalimbali, kupata maelezo kutoka kwa wataalamu wa kampuni pamoja na kunufaika na ofa maalumu zilizoandaliwa kwa kipindi cha maonesho.
Amesema maonesho hayo ni fursa muhimu kwa wananchi kujifunza kuhusu teknolojia mpya na huduma zinazotolewa na Halotel, huku akibainisha kuwa kampuni itaendelea kuwahudumia wateja kwa ubunifu na ufanisi.


