12.9 C
New York

Usiyoyajua kuhusu ugonjwa wa mkwe wa Rais Trump

Published:

WASHINGTON DC, Marekani

ALIYEWAHI kuwa mke wa mtoto wa Rais Donald Trump aitwaye Donald Trump Jr, Vanessa, amegundulika kuwa na ugonjwa wa saratani ya matiti.

Vanessa amesema alifanyiwa vipimo mapema wiki hii na ndipo alipogundulika kuwa na ugonjwa huo.

“Nashirikiana kwa karibu na madaktari wangu juu ya matibabu,” aliandika Vanessa kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram.

Bibiye huyo aliachana na Donald Trump Jr mwaka 2018 baada ya ndoa yao kuwapatia watoto watano.

Mwaka jana, Vanessa na staa wa mchezo wa gofu, Tiger Woods, walitangaza kuwa na uhusiano wa kimapenzi.

TRUMP ALIWAKUTANISHA

Vanessa aliyewahi kuwa mwanamitindo maarufu, alianza kufahamiana na Donald Trump Jr baada ya wawili hao kukutanishwa na ‘mzee’ Trump mwanzoni mwa miaka ya 2000.

Kwa mujibu wake, Vanessa anasema alikuwa kwenye onyesho la mitindo na ndipo Trump alipomfuata akiwa ameongozana na mwanaye (Donald Trump Jr).

Baada ya kufahamiana, Vanessa na Donald Trump Jr walifunga ndoa mwaka 2005 katika nyumba ya kifahari ya Trump mjini Florida.

Katika watoto wao watano, Kai Trump mwenye umri wa miaka 19 ni maarufu zaidi kwa kuwa amekuwa akionekana mara kadhaa akiwa na babu yake (Rais Trump) katika Ikulu ya Marekani.

SARATANI YA MATITI NI NINI?

Saratani ya matiti ni ugonjwa unaotokana na uzalishwaji wa seli uliokithiri katika matiti, hivyo kusababisha uvimbe.

Seli hizo huongezeka kwa kasi katika eneo linalohusika na uzalishaji wa maziwa, kabla ya kuvamia na kusambaa kwenye tishu za matiti.

Tafiti za kisayansi zinaeleza kuwa wanawake ni wahanga wakubwa kwa asilimia 80, ingawa wanaume nao hupata saratani ya matiti (0.5%-1%). Ugonjwa huo ni chanzo cha vifo zaidi ya 670,000 duniani kote.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya la Kimataifa (WHO), mkakati wa dunia ni kuhakikisha vifo vya saratani ya matiti vinapungua kwa asilimia 2.5 kufikia mwaka 2040.

Vihatarishi vyake ni pamoja na umri mkubwa (miaka zaidi ya 40), unene uliopitiliza na matumizi makubwa ya pombe na tumbaku. Inaweza pia kuwa rahisi kwa mtu anayetokea kwenye familia yenye historia ya ugonjwa huo.

Related articles

Recent articles