MANILA, Ufilipino
SERIKALI ya Ufilipino imeagiza vyombo vya dola kumtia nguvuni Seneta wake aliyefunguliwa mashitaka na Mahakama ya Uhalifu ya Kimataifa (ICC), Ronald dela Rosa.
ICC inamtaja Dela Rosa kama sehemu muhimu ya uhalifu dhidi ya binadamu wakati wa operesheni ya kutokomeza biashara ya dawa za kulevya iliyoratibiwa na Rais wa Ufilipino wakati huo, Rodrigo Duterte.
Dela Rosa, maarufu pia kwa jina la ‘Bato’ (Mwamba), alikuwa Mkuu wa jeshi la polisi katika operesheni hiyo iliyohusisha mauaji ya wale waliotajwa kufanya biashara hiyo.
Operesheni hiyo iliyohusisha matumizi ya helikopta katika maeneo korofi kwa uuzaji wa dawa za kulevya ilisababisha vifo vya maelfu ya watu na kukosolewa vikali na wanaharati wa haki za binadamu wa ndani na nje ya Taifa hilo.
Kwa sasa, Mamlaka za Ufilipino zimeeleza kuwa mwanasiasa huyo amekamatwa ili akabiliane na mashitaka yanayomkabili mbele ya ICC.


