Na Hassan Mwasha, Gazetini
MJADALA mkubwa kwa sasa katika soka la Tanzania, hasa Ligi Kuu Bara, ni kiwango bora alichonacho kiungo wa kimataifa wa Zambia, Clatous Chama, tangu arejee Simba.
Hata hivyo, kabla ya kumgusa Chama na ubora wake, kuna mambo kadhaa ya kukumbushana, ambayo yanajanga msingi wa andiko hili. Endelea kusoma.
Iko hivi; katika soka la Tanzania, wachezaji wa kigeni wamekuwa wakikumbana na changamoto kubwa nne pale wanapojiunga na klabu kongwe za Simba na Yanga.
Mosi, ni kuthibitisha ubora waliotoka nao huko walikokuwa wakicheza. Wengi walikuja wakiwa na viwango bora lakini Ligi ya Bongo na presha ya kucheza timu hizo iliwashinda, wakaondoka zao.
Pili, ni kuingia kwenye mioyo ya mashabiki wa klabu waliyojiunga nayo. Katika hili, wapo ambao hawakufanikiwa kuonesha viwango vikubwa lakini ilitokea tu wakawa vipenzi vya mashabiki wa timu zao. Unamkumbuka Skudu Makudubela? Ni miongoni mwao.
Tatu, hata kama mchezaji atakuwa na kiwango kizuri na kupendwa na mashabiki wake wa Simba/Yanga, mtihani atakaokuwa nao ni kuushawishi upande wa pili nao umkubali. Si wachezaji wengi waliofanikiwa katika eneo hilo.
Nne, kuna ‘ishu’ ya kuwa na mwendelezo wa kiwango bora ndani ya uwanja. Ni eneo jingine gumu kwa mchezaji kufaulu, si tu hapa Bongo, bali hata duniani kwa ujumla.

Tujikumbushe; ni ‘maproo’ wangapi walikuja nchini kujiunga na Simba au Yanga wakiwa wa moto lakini ‘wakapotea’ mazima ndani ya misimu isiyozidi miwili? Ni wengi.
Katika vizingiti vinne hivyo, ndipo unapoikuta picha halisi ya kiungo wa Simba raia wa Zambia, Clatous Chama. ‘Mwamba wa Lusaka’ amefaulu katika maeneo yote yaliyotajwa hapo juu. Nitaeleza.
Chama alijiunga na Simba akiwa mchezaji mwenye ‘profile’ kubwa katika Ligi Kuu ya Zambia. Alipofika Bongo, moto ukawa ni ule ule. Alifanikiwa kuhamishia makali yake katika soka la Tanzania.
Pia, katika kizingiti cha pili cha kukubalika kwa mashabiki wake, hilo halina ubishi. Kwa miaka yote aliyocheza Simba na hata alipoondoka na kwenda Yanga na Singida Black Stars, bado alibaki kwenye mioyo ya Wanasimba.
Unaweza kuzungumzia kauli za kejeli juu ya umri wake walizozitoa mashabiki wa Simba wakati alipoondoka, lakini ukweli ni kwamba zilizotokana na hasira na wivu wa kuona wapinzani wao wamepata silaha ya maangamizi.
Tutadanganyana kuamini kuwa upendo wa mashabiki wa Simba kwa Chama umewahi kupotea kwa namna yoyote ile, hata pale ilipotokea akacheza chini ya kiwango au kuonesha vitendo vya utovu wa nidhamu ndani na nje ya uwanja.

Mashabiki walibaki upande wake siku zote. Kwa ufupi, amefanikiwa kujenga ‘brand’ yake ndani ya mioyo ya mashabiki na hata viongozi wa klabu hiyo. Hata aliporejea, alipokewa kwa ‘vibe’ kubwa, kana kwamba hakuwahi kuitwa ‘mzee’.
Wakati huo huo, Chama amefanikiwa kuvuna ushawishi upande wa pili. Licha ya kumtolea kauli za kejeli kuhusiana na umri alipokuwa Simba, Yanga ilimsajili na mashabiki wa timu hiyo walimpokea kwa shangwe kubwa, kana kwamba ni kinda wa ‘U-17’.
Hiyo ilitosha kabisa kuthibitisha kuwa Chama alishapenya kuwa kujenga hema la makazi kwenye mioyo yao. Kwamba kelele za umri zilitokana na aidha wivu au hasira kwa kuona wapinzani wao wanafaidi.
Kwa upande wa mwendelezo wa ubora, ni eneo jingine alilofaulu Chama. Kwa miaka zaidi ya 10 aliyocheza Tanzania, ni mechi za kuhesabika mno unazoweza kusema Chama hakuwa na mchango ndani ya uwanja.
Mathalan, Simba ilipofanya makubwa ndani na nje ya nchi, ikiwamo kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu misimu minne mfululizo na kufika robo fainali kadhaa za Ligi ya Mabingwa Afrika, Chama alikuwa ‘injini’ ya timu, hasa kwenye nyakati ngumu zilizohitaji uwezo binafsi wa mchezaji.


