Na mwandishi wetu, Gazetini
SERIKALI imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji katika sekta ya usafiri wa anga kwa kuimarisha miundombinu ya viwanja vya ndege, hatua iliyochangia kuvutia mashirika saba mapya ya ndege ya kimataifa kuanzisha safari nchini na kuongeza ushindani wa kibiashara.
Kupitia Wizara ya Uchukuzi na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), mashirika yaliyoanza au kupanua huduma zake nchini ni Airlink, Zambia Airways, Saudia, Air France, Skyward Express, South African Airways na Xerin Air.
Msemaji Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Februari 26, 2026, amesema hatua hiyo imeongeza chaguo za usafiri wa kimataifa, kurahisisha safari za abiria na mizigo pamoja na kuchochea ukuaji wa sekta za utalii na biashara.
Amesema maboresho ya miundombinu na mifumo ya usalama pia yameziwezesha Viwanja vya Ndege vya Kimataifa vya Julius Nyerere (JNIA) na Kilimanjaro (KIA) kutambuliwa kimataifa kwa ubora na usalama.
“Hatua hizi zimeimarisha ushindani wa sekta ya anga, zimeongeza idadi ya mashirika ya ndege yanayofanya safari nchini na zimefungua fursa zaidi za ukuaji wa utalii na biashara,” amesema Msigwa.
Wakati huo huo, takwimu za TAA zinaonesha kuimarika kwa utendaji wa sekta hiyo katika mwaka wa fedha 2024/2025 ikilinganishwa na mwaka wa fedha 2023/2024, ambapo idadi ya safari za ndege iliongezeka kutoka safari 148,897 hadi 149,835, sawa na ongezeko la asilimia 0.6.
Kwa upande wa abiria, idadi imeongezeka kutoka milioni 5.15 hadi milioni 5.25, ikiwa ni ongezeko la asilimia 2.0, huku mizigo ikiongezeka kwa kasi zaidi kutoka tani 34,620 hadi tani 37,683, sawa na ongezeko la asilimia 8.8.
Katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2025, sekta hiyo imeendelea kuonesha mwelekeo chanya ambapo safari za ndege ziliongezeka kwa asilimia 10 kutoka safari 83,647 hadi 91,760, huku idadi ya abiria ikiongezeka kwa asilimia 9 kutoka 2,819,912 hadi 3,071,081.
Ongezeko hilo linaashiria kuimarika kwa shughuli za kiuchumi, ukuaji wa biashara na kuongezeka kwa mahitaji ya usafiri wa anga, huku Serikali ikiendelea kuboresha miundombinu ili kuvutia uwekezaji zaidi na kukuza mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa taifa.


