LONDON, Uingereza
WAZIRI Mkuu wa Uingereza, Sir Keir Starmer, amesema serikali yake itashirikiana kwa karibu na sekta zilizoathirika pamoja na washirika wa kimataifa ili kukabiliana na athari zozote zinazoweza kujitokeza kutokana na mvutano wa kisiasa unaoendelea duniani.
Akizungumza na waandishi wa habari, Starmer ameeleza kuwa serikali inafuatilia kwa karibu madhara ya kiuchumi yanayotokana na vita, hususan yale yanayohusiana na miundombinu ya mafuta na gesi pamoja na usafirishaji wa nishati kupitia Ghuba ya Hormuz.
Amesema Uingereza tayari ina mpango madhubuti wa kupunguza utegemezi wake kwenye masoko hatarishi ya nishati na kujenga kile alichokiita “usalama wa nishati na uhuru wa nishati tunaouhitaji.”
Starmer pia ameonya kuhusu hatari ya baadhi ya watu kutumia hali ya kisiasa ya sasa duniani kuchochea mgawanyiko ndani ya jamii.
“Ni jambo la kusikitisha kwamba kuna wanaoweza kutumia mazingira haya ya kisiasa kututenganisha,” amesema.
Ameongeza kuwa serikali inaendelea kuwasiliana na jamii mbalimbali nchini humo, hususan za Wayahudi na Waislamu, ili kuhakikisha wanapata msaada unaofaa wakati huu wa taharuki.
Kwa mujibu wa Starmer, ni muhimu kwa jamii kushikamana katika kipindi hiki, akibainisha kuwa raia wa Uingereza waliokwama katika maeneo yenye machafuko wanatoka katika makundi tofauti ya kijamii.
“Jamii inapaswa kushikamana wakati huu. Raia wetu waliokwama katika ukanda huo wanatoka katika makundi yote ya kijamii, na hata vikosi vya ulinzi vinavyowalinda vinatoka katika asili zote,” amesisitiza.
Waziri Mkuu huyo pia amefafanua kuwa moja ya malengo makuu ya mkutano wake na waandishi wa habari lilikuwa kuwahakikishia wananchi na kupunguza hofu iliyojitokeza miongoni mwa umma kuhusu hali ya usalama duniani.
Aidha, Starmer ametetea uamuzi wa Uingereza kutoshiriki katika mashambulizi ya awali yaliyofanywa na Marekani na Israel dhidi ya Iran, pamoja na kukataa ombi la Marekani la kuruhusu ndege zake kutumia vituo vya jeshi la Uingereza kwa ajili ya mashambulizi ya uvamizi.


