9.5 C
New York

Maktaba| Kiti kilivyosababisha ‘bifu’ la Henry, Nasri

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

MAKTABA ni safu mpya itakayokuwa ikikujia kupitia hapa GAZETINI, ikilenga kukupa simulizi za mikasa ya ndani na nje ya uwanja ya mastaa wa zamani wa soka, kikapu, ndondi, na hata muziki.

Leo, tunafingua MAKTABA yetu kwa kuwaangazia Samir Nasri, Thierry Henry na William Gallas, ikielezwa kuwa hawakuwa wakiiva chungu kimoja wakati wote walipokuwa wakicheza pamoja timu ya taifa ya Ufaransa.

Tuazie na ‘bifu’ la Nasri na Henry. Ni ugomvi unaotajwa kuanza msimu wa 2007-2008. Stori inaanzia katika kambi ya timu ya taifa ya Ufaransa wakati wa kujiandaa na mashindano ya Euro ya mwaka 2008.

Wakati huo, Nasri ilikuwa ndiyo mara yake ya kwanza kuitwa timu ya taifa lakini Henry tayari alishakuwa mzoefu na nahodha wa kikosi.

Unajua kilichosababisha ugomvi? Ni kitendo cha Nasri kuchukua na kukalia kiti cha Henry. Ni kiti ambacho mara zote alikitumia Henry akiwa timu ya taifa.

Ingawa Nasri alisema hakufanya kwa nia ya kumkosea adabu, Gallas akisimulia tukio hilo, alisema Henry alihisi kuvunjiwa heshima na kuanzia hapo uhusiano wake na ‘dogo’ ulianza kuwa mbaya.

Kama hiyo haitoshi, lipo tukio jingine lililozidisha ‘uadui’ wa Nasri na mkongwe huyo kila walipokutana kwenye kambi ya timu ya taifa.

Kwa muda mrefu, hata kabla ya Nasri kuanza kuitwa kikosini, ulikuwapo utaratibu wa wachezaji wachanga kusimama pindi Henry alipokuwa akiingia kwenye chumba cha kubadilishia nguo.

Haikuwa kuwadhalilisha, bali ishara ya heshima kwa umri, uwezo na mafanikio makubwa aliyokuwa nayo Henry.

Kwa Nasri, ni kama utamaduni huo ulikuwa ukimpa tabu, kabla ya kuamua kutosimama. Kitendo hicho  kilimfanya Henry amuone Nasri kuwa ni kijana mwenye kiburi. Ikaongeza uhusiano mbaya kati yao.

Haikuishia kwa Henry. Baadaye, Nasri aliingia kwenye bifu zito na mkongwe mwingine, Gallas. Ni ugomvi uliodumu kwa miaka miwili, kuanzia mwaka 2008 hadi 2010.

Chanzo ni kitabu alichoandika Gallas kilichopewa jina la ‘The Secret’ (Siri). Ndani yake, alimzungumzia vibaya Nasri akimtaja kuwa ni mchezaji mwenye tabia isiyofaa na aliyekosa nidhamu.

Kauli hizo zilimchefua Nasri na kusababisha wawili hao kutoongea kwa muda mrefu, hata walipokutana ana kwa ana wakiwa kwenye kambi ya timu ya taifa.

Kikosi cha Ufaransa (EURO 2008)

Makipa: Gregory Coupet, Sebastien Frey, Steve Mandanda.

Mabeki: Gallas, Lilian Thuram, Eric Abidal, Willy Sagnol, Patrice Evra,Jean-Alain Boumsong, Francois Clerc.

Viungo: Claude Makelele, Patrick Vieira, Alou Diarra, Lassana Diarra, Jeremy Toulalan, Samir Nasri, Florent Malouda.

Washambuliaji: Henry, Karim Benzema, Nicolas Anelka, Franck Ribery, Sidney Govou.

Maoni: 0689 379 993

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img