Na mwandishi wetu, Gazetini
BENKI za NMB na CRDB zimeendelea kuthibitisha ubora na uimara wao katika sekta ya fedha nchini baada ya kila moja kutangaza faida kabla ya kodi (Profit Before Tax – PBT) inayozidi Sh trilioni 1, hatua inayozidi kuimarisha nafasi yao kama nguzo kuu za sekta ya benki Tanzania.
Kwa pamoja, benki hizo mbili zinachangia zaidi ya nusu ya faida yote ya sekta ya benki nchini inayokadiriwa kufikia Sh trilioni 2.4, jambo linaloonesha ukubwa wa mchango wao katika uchumi wa taifa.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa, Benki ya NMB imeongoza kwa upande wa faida kabla ya kodi kwa kupata Sh trilioni 1.13, huku faida baada ya kodi (PAT) ikifikia Sh bilioni 749.7. CRDB nayo ilipata faida kabla ya kodi ya Sh trilioni 1.0 na faida baada ya kodi ya Sh bilioni 724.6.
Kwa upande wa ukubwa wa mali (assets), CRDB imeendelea kuongoza ikiwa na mali zenye thamani ya Sh trilioni 22.2 ikilinganishwa na Sh trilioni 17.2 za NMB. CRDB pia inaongoza katika kiwango cha amana za wateja kilichofikia Sh trilioni 14.8, huku NMB ikikusanya Sh trilioni 12.4.
Katika mikopo iliyotolewa kwa wateja, CRDB ina mkoba wa mikopo wa Sh trilioni 13.7, wakati NMB ina Sh trilioni 10.4, ishara ya mchango mkubwa wa benki hizo katika kufadhili shughuli za kiuchumi.
Hata hivyo, NMB imeonesha uimara zaidi katika udhibiti wa mikopo chechefu (NPLs) kwa kuwa na kiwango cha asilimia 2.5 ikilinganishwa na asilimia 3.0 cha CRDB.
CRDB inaongoza pia kwa idadi ya wafanyakazi 4,528 na matawi 261, ikilinganishwa na wafanyakazi 4,088 na matawi 248 ya NMB.
Kwa ujumla, takwimu zinaonesha ushindani wa kipekee kati ya benki hizo mbili, ambapo CRDB inaongoza kwa ukubwa na mtandao mpana, huku NMB ikijipambanua kwa ufanisi wa faida na usimamizi wa hatari, hali inayozidi kuimarisha sekta ya benki nchini.


