10.5 C
New York

Senegal v Misri … Mane, Salah wana vita ya kisasi AFCON 2025

Published:

RABAT, Morocco

UKIACHA vita ya Nigeria na Morocco, nusu fainali nyingine kali msimu huu wa fainali za AFCON ni ile itakayozikutanisha Senegal dhidi ya Misri.

Ratiba inaonesha kuwa mechi mbili za kukata na shoka za hatua hiyo zitachezwa Jumatano hii, kwa maana ya Januari 14, 2026.

Senegal dhidi ya Misri ni vita ya kisasi kwa mataifa hayo, pia itakayowakutanisha mastaa wawili wakubwa, Sadio Mane wa Senegal na Mohamed Salah wa Misri.

Kwanini ni vita ya kisasi? Senegal walipochukua kwa mara ya kwanza ubingwa wa AFCON mwaka 2021, waliifunga Misri katika mchezo wa fainali.

Ni mchezo uliomalizika kwa suluhu (0-0), kabla ya Senegal ‘Simba wa Teranga’ kubeba taji kwa ushindi wa mikwaju ya penalti.

Safari hii, Misri watarejea wakiwa na hasira si tu ya kulipiza kisasi, bali pia kutwaa ubingwa wao wa kwanza wa AFCON baada ya kukosa kwa miaka zaidi ya 10.

Ikumbukwe, Senegal imefika hatua hii kwa kuifunga Mali bao 1-0 katika hatua ya robo fainali, mfungaji akiwa ni Iliman Ndiaye.

Ni mchezo ambao Mali waliumaliza wakiwa 10 uwanjani baada ya kiungo wao anayekipiga Tottenham, Yves Bissouma, kulimwa kadi nyekundu.

Kwa upande wao, Misri ‘Mafarao’ walivuka robo fainali kwa kuwasukuma nje ya mashindano mabingwa watetezi, Ivory Coast, wakiifunga mabao 3-2.

Salah ndiye aliyefunga bao la ushindi baada ya Rami Rabia na Omar Marmoush nao kuifungia Misri. Ivory Coast walipata bao la kujifunga, kabla ya Guela Doue naye kuzitikisa nyavu za Mafarao.

Kuelekea nusu fainali yao, Senegal na Misri zimekutana mara nne, ambapo kila moja imepata ushindi mara mbili.

Mara ya mwisho kwa vigogo hao kuvaana ilikuwa mwaka 2021, ambapo Senegal ilishinda kwa penalti na kutwaa kwa mara ya kwanza ubingwa wa fainali za AFCON.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img