11.6 C
New York

Siku 34 za msako wa Maduro, hatimaye Marekani imemtia mkononi

Published:

WASHINGTON DC, Marekani

BAADA ya miezi mingi ya Marekani kuzishambulia kwa risasi na mabonu boti za Venezuela kwa madai ya kusafirisha dawa za kulevya, hatimaye imefanikiwa kumtia mkononi Rais wa Taifa hilo, Nicolas Maduro.

Kabla ya Marekani kuishambulia Venezuela na hatimaye kumkamata Maduro, Rais Donald Trump alikuwa akimshutumu si tu kwa madai ya utawala wa kidikteta, bali pia kujihusisha na biashara hiyo.

Maduro amekuwa akikanusha na kuzua vita kali ya maneno kati yake na Trump. Kwa mujibu wa Maduro, shutuma za Marekani dhidi yake ni sehemu ya jitihada za kumtoa madarakani.

Hata hivyo, vikosi vya kijeshi vya Marekani kuishambulia Venezuela na kisha kumkamata Maduro ni matokeo ya mkakati wao wa muda mrefu. Makala haya yanachambua zaidi.

Januari 20, 2025

Trump alisaini agizo la kuyatambua magenge ya uhalifu ya Venezuela kama ‘taasisi za kigaidi za kimataifa’. Baadhi ya magenge hayo ni lile la mtaani linalofahamika kwa jina la Tren de Aragua.

Licha ya Trump kusema Maduro anashirikiana na Tren de Aragua, mashirika ya kijasusi ya Marekani yalikanusha na kusema kiongozi huyo hajihuishi na genge hilo.

Februari 20, 2025

Serikali ya Trump iliyatangaza magenge nane ya uhalifu ya Venezuela katika orodha ya vikundi hatarishi vya kigaidi vya kimataifa.

Ni kwa kuyahusisha magenge hayo na kile kinachofanywa na makundi ya Al-Qaeda na Islamic State (IS).

Septemba 2, 2025

Marekani ilishambulia kwa mara ya kwanza boti ya Venezuela kwa kile Trump alichodai kuwa ilikuwa imebeba dawa za kulevya zilizokuwa zikisafirishwa na genge la Tren de Aragua.

Kwa mujibu wa Trump, watu wote 11 waliokuwa kwenye boti hiyo walipoteza maisha. Hakuishia kusema tu, bali pia aliposti video fupi ya shambulio hilo.

Septemba 10, 2025

Bunge la Marekani lilipeleka barua yake Ikulu ya Marekani likilaani kile kilichotokea. Shambulizi la boti ya Venezuela la Septemba 2.

Seneta wa Kisiwa cha Rhode, Jack Reed, alisema jeshi la Marekani lilikwenda kinyume cha sheria kwa kitendo cha kushambulia na kuua, badala ya kuwakamata na kuwafungulia mashitaka hao waliotajwa kuwa ni wahalifu.

Septemba 15, 2025

Vikosi vya Marekani vilifanya shambulio la pili kwa meli za Venezuela, sababu ikiwa ni ile ile, kwamba ilikuwa na dawa za kulevya. Watu watatu waliuawa katika tukio hilo.

Alipopulizwa kama kuna ushahidi wa kuthibitisha kuwa boti hiyo ilikuwa na dawa za kulevya, Trump alidai kuwa wahalifu hao walizimwaga baharini.

Hata hivyo, si jeshi wala Ikulu ya Marekani iliyokuja na video ikionesha dawa hizo zikiwa zimetupwa baharini.

Septemba 19, 2025

Kwa mara ya tatu, Trump akitangaza kuwa vikosi vyake vimetekeleza shambulizi dhidi ya boti nyingine ya Venezuela.

Si tu maseneta wa Marekani, bali pia wanaharakati wa haki za binadamu waliibuka na kulaani hatua hiyo.

Oktoba 3, 2025

Siku moja baada ya Trump kusema Marekani imeingia kwenye vita dhidi ya magenge ya uhalifu ya Venezuela, Katibu Mkuu wa Wizara ya ulinzi, Pete Hegseth, naye aliibuka.

Hegseth alisema ameagiza boti ya Venezuela kushambuliwa, akidai kuwa ilikuwa imebeba dawa za kulevya ‘unga’.

Oktoba 8, 2025

Wabunge wa Chama cha Republican walikuja juu na kutoa tamko zito la kuibana Serikali ya Trump juu ya kile inachokifanya kwa Venezuela.

Katika azimio lao, wabunge hao walitaka Rais Trump kuomba ridhaa Bungeni kila anapotaka kutekeleza shambulizi lolote.

Oktoba 14, 2025

Trump akitangaza kuwa Marekani imefanya shambulizi jingine kwa boti ya Venezuela. Ikumbukwe, hilo lilikuwa ni shambulizi la sita.

Katika taarifa yake, alisema shambulizi hilo dhidi ya boti ndogo iliyokuwa na dawa za kulevya lilisababisha vifo vya watu sita.

Oktoba 15, 2025

Trump alithibitisha kuwa amelitaka Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) kuingia na kuendesha operesheni nchini Venezuela.

Hata hivyo, kwa wakati huo, Trump hakusema kama aliwaagiza pia CIA kumshughulikia Rais wa Taifa hilo, Maduro.

Oktoba 16, 2025

Trump alisema Marekani imeishambulia boti nyingine ya Venezuela na kusababisha vifo vya watu wawili.

Oktoba 17, 2025

Wanajeshi wa Marekani waliishambulia boti nyingine ya Venezuela kwa madai kuwa ilikuwa na dawa za kulevya aina ya narcotics.

Marekani ilidai kuwa meli hiyo ilikuwa mali ya kund la waasi nchini Colombia, National Liberation Army (ELN). Watu watatu walifariki.

Oktoba 21, 2025

Marekani ilitangaza shambulizi la nane dhidi ya boti ya Venezuela ikiwa Mashariki mwa Bahari ya Pacific na kusababisha vifo vya watu wawili.

Oktoba 22, 2025

Ni siku ambayo kwa mara nyingine Serikali ya Marekani ilitangaza kuua watu watatu iliposhambulia boti nyingine ya Venezuela huko Mashariki mwa Pacific. Hilo lilikuwa ni shambulizi la tisa.

Oktoba 24, 2025

Ikulu ya Marekani ilitangaza kufanya shambulizi la 10 dhidi ya boti za Venezuela. Safari hii, taarifa ya Ikulu ilieleza kuwa ni shambulizi lililoua watu sita. Kwa mujibu wake, ni boti iliyokuwa na dawa za kulevya.

Oktoba 31, 2025

Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa upande wa utetezi wa haki za binadamu, Volker Türk, aliitisha uchunguzi dhidi ya mashambulizi ya Marekani kwa boti za Venezuela.

Kupitia kwa Msemaji wake, Ravina Shamdasani, Turk alisema: “Marekani inapaswa kuchukua hatua juu ya mauaji yanayoendelea katika mashambulizi hayo.”

Novemba Mosi, 2025

Kwa mara nyingine, Ikulu ya Marekani iliibuka na taarifa kuwa vikosi vyake vimetekeleza shambulizi dhidi ya ‘boti ya Venezuela yenye dawa za kulevya’. Watu watatu walifariki.

Novemba 11, 2025

Serikali ya Venezuela ilitoa tamko ikidai kuwa imejipanga kukabiliana na Marekani endapo mazingira yatalazimisha mataifa hayo kuingia vitani. Kauli ya Waziri wa Ulinzi, Vladimir Padrino Lopez.

Novemba 15, 2025

Watu watatu waliuawa wakati vikosi vya Marekani vilipoishambulia boti ya Venezuela. Kwa mujibu wa Marekani, lilikuwa ni shambulizi la 21 dhidi ya boti za usafirishaji wa dawa za kulevya.

Novemba 16, 2025

Trump aliibuka na kusema huenda kukawa na mazungumzo kati yake na Maduro. Kwa mujibu wake, Venezuela ingevutiwa na mazungumzo hayo.

Desemba 4, 2025

Zilikuwepo taarifa za wanajeshi wa Marekani kuua watu wanne katika shambulizi lao dhidi ya boti ya Venezuela huko Mashariki mwa Pacific.

Desemba 10, 2025

Marekani ilitangaza kushikilia meli kubwa ya mafuta ya Venezuela. Ni saa chache tu baada ya meli hiyo kuanza safari ikiwa na mapipa takribani milioni mbili.

Wakati huo, Mwanasheria Mkuu wa Marekani, Pam Bondi, alidai kuwa meli hiyo ilikuwa chini ya moja ya magenge ya uhalifu wa biashara ya dawa za kulevya nchini Venezuela.

Desemba 15, 2025

Jeshi la Marekani lilikua watu nane baada ya kushambulia boti ya Venezuela huko Mashariki mwa Pacific. Madai yakiwa ni yale yale, ilikuwa ikisafirisha ‘unga’.

Desemba 16, 2025

Trump alisema ameagiza kukamatwa kwa meli zote za mafuta zilizokuwa zikitoka na kuingia Venezuela. Hatua hiyo ilitafsiriwa kuwa ni mpango wake wa ‘kuua’ uchumi wa nchi hiyo unaotegemea zaidi mafuta.

Desemba 17, 2025

Marekani ilikiri kuhusika katika shambulizi dhidi ya boti ya Venezuela na kuua watu wanne iliowataja kuwa ni wasafirishaji wa dawa za kulevya. Bunge la Marekani liliamka na kutaka Trump adhibitiwe kisheria juu ya matumizi yake ya jeshi.

Desemba 18, 2025

Serikali ya Marekani ilithibitisha kufanya mashambulizi mawili dhidi ya boti za Venezuela. Watu watano walipoteza maisha, huku Marekani ikiwataja kuwa ni wasafirishaji wa dawa za kulevya.

Desemba 20, 2025

Marekani kupitia kwa Wizara ya Ulinzi ilikiri kusimamisha meli ya mafuta ya Venezuela. Siku mbili baadaye, ikaibuka taarifa ya watu wanne kuuawa wakati Marekani iliposhambulia boti ya Venezuela.

Desemba 29, 2025

Trump aliibuka na madai kuwa Marekani imenasa kituo kinachozihudumia meli za dawa za kulevya za Venezuela. Hata hivyo, hakutaja kilipo kituo hicho, kama ni Venezuela au nje ya nchi hiyo.

Desemba 30, 2025

CIA walitangaza kufanya shambulizi la ndege zisizo na rubani katika eneo walilotaja kuwa ni kitovu cha magenge ya uhalifu nchini Venezuela.

Haa hivyo, Serikaki ya Venezuela haikuthibitisha kutokea kwa tukio hilo. Pia, idadi ya vifo haikuwekwa hadharani wakati huo.

Desemba 30, 2025

Vikosi vya jeshi la Marekani vilishambulia boti tatu za Venezuela. Watu wawili walifariki na wengine walilazimika kujitosa kwenye maji.

Desemba 31, 2025

Serikali ya Marekani ilitangaza kuziwekea vikwazo kampuni nne za mafuta zilizoko nchini Venezuela. Pia, adhabu hiyo iliambatana na ile ya kushikilia meli nne za mafuta.

Desemba 31, 2025

Marekani kupitia kwa Wizara ya Ulinzi ilitangaza kuua watu watano katika shambulizi dhidi ya boti mbili za Venezuela. Ni kwa madai ya boti hizo kubeba dawa za kulevya.

Januari 1, 2026

Katika salamu zake za Mwaka Mpya, Rais wa Venezuela, Maduro, alihutubia Taifa kupitia televisheni. Alisema wako tayari kushirikiana na Marekani katika vita dhidi ya dawa za kulevya.

Aidha, Maduro ambaye alisema mpango wa Marekani ni kumtoa madarakani ili kupata nafasi ya kuingia Venezuela na kujichotea rasilimali za nchi yake.

Januari 3, 2025

Marekani ilifanya shambulizi kubwa katika Mji Mkuu wa Venezuela wa Caracas. Taarifa zinasema shambulizi hilo limefanikisha kukamatwa kwa Maduro na mkewe, Flores.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya habari, wawili hao kwa sasa wanashikiliwa na Marekani mjini New York.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img