10.5 C
New York

Mastaa 10 wenye pesa ndefu AFCON 2025

Published:

RABAT, Morocco

KARNE hii ya 21 imeshuhudia vipaji vikubwa vya soka barani Afrika na sasa wanaoneshana kazi katika fainali za Mataifa ya Afrika za mwaka huu (AFCON 2025) zinazoendelea nchini Morocco.

Michuano hiyo ilianza Desemba 21 na inatarajiwa kufikia ukomo Januari 18, mwakani. Sasa, kwa kuwa tayari kuna mastaa wengi wanaoyawakilisha mataifa yao huko Morocco, makala haya yanakuibulia 10 wanaolipwa mishahara minono katika klabu zao.

Riyad Mahrez (Algeria)

Safari ya ukubwa wa jina lake ilianzia Leicester City. Nyota huyo raia wa Algeria alisajiliwa na klabu hiyo ya England mwaka 2014.

Baada ya misimu kadhaa akiwa na Manchester City, Mahrez kwa sasa anacheza Saudi Arabia na mshahara wake ni Pauni 827,448 kwa wiki.

Sadio Mane (Senegal)

Mane, tofauti na wachezaji wengi wanaolipwa vizuri, huwa hana mambo mengi nje ya uwanja. Anakipiga Al-Nassr ya Saudia, akiwa na Cristiano Ronaldo klabuni hapo.

Kwa wiki, Mane aliyewahi kuwika akiwa na Liverpool na Bayern Munich, amekuwa na uhakika wa kuingiza kwenye akaunti yake ya benki kitita cha Pauni 634,060.

Kalidou Koulibaly (Senegal)

Beki wa zamani wa Chelsea, ambaye ni miongoni mwa mastaa wa soka walioondoka Ulaya na kutimkia Saudi Arabia. Koulibaly mwenye umri wa miaka 34, kwa sasa anatumikia Al Hilal na mshahara wake ni Pauni 550,047 kwa wiki.

Mohamed Salah (Misri)

Kwa miaka mingi ya hivi karibuni, ‘Mo’ Salah amekuwa mfalme, si tu kwa klabu yake ya Liverpool, bali pia hata timu ya taifa ya Misri.

Liverpool wanamlipa Pauni 400,000 kwa wiki na ni baada ya mkataba wa miaka miwili aliosaini mwishoni mwa msimu uliopita klabuni hapo.

Victor Osimhen (Nigeria)

Mbali ya kazi kubwa anayoifanya akiwa Galatasaray ya Uturuki, mshambuliaji wa kati huyo pia ndiye tegemeo kwenye safu ya ushambuliaji ya timu yake ya taifa ya Nigeria ‘Super Eagles’.

Osimhen ni miongoni mwa wanasoka wenye mishahara minono katika fainali za AFCON za mwaka huu. Analipwa Pauni 318,450 kila wiki.

Omar Marmoush (Misri)

Alisajiliwa na Manchester City mwanzoni mwa mwaka huu ili kuiongezea makali safu ya ushambuliaji inayoongozwa na Erling Haaland.

Marmoush aliyetokea Eintracht Frankfurt ya Bundesliga, analipwa Pauni 295,000 kwa wiki akiwa na matajiri hao wa jijini Manchester.

Franck Kessie (Ivory Coast)

Kiungo huyo alipata umaarufu akiwa na AC Milan, kabla ya mabosi wa Barcelona kumsajili mwaka 2022, ambapo hata hivyo hakung’ara klabuni hapo.

Kwa sasa, Kessie anakipiga Al Ahli ya Ligi Kuu ya Saudi Arabia, akiripotiwa kuingiza Pauni 273,442 kwa wiki klabuni hapo.

Achraf Hakimi (Morocco)

Kwa miaka 10 ya hivi karibuni, Hakimi ni mchezaji pekee wa eneo la ulinzi aliyekaribia zaidi kuibeba tuzo ya Ballon d’Or.

Kutokana na kiwango chake kikubwa akiwa PSG, matajiri wa klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) wanamlipa Pauni 231,662 kwa wiki.

Edouard Mendy (Senegal)

Wakati fulani, Mendy aliwahi kutajwa kuwa mmoja ya makipa bora zaidi duniani. Alicheza kwa muda mfupi Chelsea, kabla ya kutimkia Saudi Arabia.

Kwa sasa, Mendy ni miongoni mwa wachezaji wanaolipwa mishahara minono Ligi Kuu ya nchi hiyo, akiwa anapokea Pauni 203,808 kwa wiki.

Yassine Bounou (Morocco)

Ni kipa chaguo la kwanza katika kikosi cha timu ya taifa ya Morocco. Bounou aliwahi kuitumikia Sevilla na sasa ni mwajirwa wa Al-Hilal ya Saudi Arabia.

Kipa huyo aliyekuwa nyota wa mchezo wakati Sevilla inatwaa taji la Ligi ya Europa kwa kuifunga AS Roma msimu uliopita, analipwa Pauni 158,515 kwa wiki.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img