Na Mwandishi Wetu, Gazetini
SERIKALI imeendelea kuimarisha sekta ya nishati kupitia uwekezaji mkubwa wa zaidi ya Sh trilioni 13.5 katika miradi 41 ya umeme nchini, sambamba na uzinduzi wa mita janja za kisasa zitakazorahisisha upatikanaji wa huduma kwa Watanzania.
Kwa mujibu wa Wizara ya Nishati, kati ya miradi hiyo 41, sita ni ya uzalishaji wa umeme na 35 ni ya usambazaji-hatua inayotajwa kuwa msingi muhimu wa mageuzi ya kiufundi na kiutendaji ndani ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO). Mageuzi hayo pia yanachukuliwa kama suluhisho kwa changamoto za muda mrefu zilizokuwa zikiwakabili watumiaji.

Akizungumza Desemba 5, jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa matumizi ya mita janja, Waziri wa Nishati Deogratius Ndejembi alisema uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita unaonesha dhamira ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha Watanzania wanapata huduma ya umeme wa uhakika, wa kisasa na unaoendana na maendeleo ya kiteknolojia.
“Mita janja ni moja ya matokeo ya uwekezaji huu mkubwa. Ni mita za kisasa zinazotoa taarifa za matumizi kwa muda halisi na kuongeza uwazi katika matumizi ya umeme,” alisema Ndejembi.
Ameeleza kuwa mita hizo mpya zitamaliza malalamiko yaliyodumu kwa miaka mingi kuhusu mita za zamani zilizokuwa zikikwama, kupoteza kumbukumbu, kutoa taarifa zisizo sahihi au kuwafanya wananchi kupanda ngazi kila wanapohitaji kuingiza tokeni.
“Mita janja itamuwezesha mteja kununua umeme akiwa mahali popote bila kulazimika kufika nyumbani. Hii itarahisisha upangaji wa bajeti, ufuatiliaji wa matumizi na kuboresha kwa ujumla mahusiano kati ya mteja na mtoa huduma,” alisema.
Utekelezaji wa miradi hiyo 41 unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika nchini, kupunguza changamoto za upotevu wa nishati, pamoja na kuimarisha uwezo wa mtandao wa usambazaji katika kukidhi kasi ya maendeleo ya uchumi wa taifa.


