Na Mwandishi Wetu, Gazetini
WAANDISHI wa habari nchini wameaswa kuwa mstari wa mbele katika kusaidia jamii, hususan ile inayoishi kandokando ya ukanda wa pwani, kutambua na kuelewa manufaa yanayopatikana kutokana na rasilimali za bahari.
Wito huo umetolewa hivi karibuni na Mhadhiri Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Idara ya Zuolojia na Uhifadhi wa Viumbe Pori, Dk. Jestina Katandukila, wakati akizungumza na GAZETINI, kando ya warsha ya kuwajengea uwezo wa waandishi wa habari za mazingira iliyofanyika jijini Tanga.
Mafunzo hayo yameandaliwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ Tanzania) pamoja na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET).

Dk. Jestina amesema bahari ina manufaa mengi ambayo bado hayajaelezwa vya kutosha kwa wananchi, hususan wale wanaoishi kandokando yake, ambapo wengi wao wamekuwa wakiitumia bahari kwa ajili ya kupata kitoweo pekee.
“Ni wakati sasa wa waandishi wa habari kutumia kalamu zenu kuielimisha jamii kuhusu nafasi ya bahari katika maisha yao. Wananchi wengi wanaamini kwamba msaada wa bahari ni samaki pekee, jambo ambalo si sahihi.
Tuwaeleze kwamba kupitia bahari wanaweza kushiriki shughuli za uhifadhi, hatua itakayochochea utalii na kuwapatia kipato cha kujikimu,” amesema Dk. Jestina.
Ameongeza kuwa elimu kuhusu masuala ya bahari inaweza kusaidia jamii kujua namna ya kukabiliana na majanga ya asili kama vile vimbunga na mmomonyoko wa pwani.
“Tunapozungumzia bahari, hatumaanishi chakula pekee. Tunamaanisha uchumi, ajira, utalii na mustakabali wa maisha ya vizazi vijavyo. Bahari ni uhai, lakini faida zake zinabaki kufichika kwa sababu ya ukosefu wa elimu sahihi,” ameongeza Dk. Jestina.
Mafunzo hayo, yanayotekelezwa kupitia Mradi wa Pwani Yetu, yanalenga kujenga uwezo wa waandishi wa habari na wataalamu wa vyombo vya habari katika uandishi wa hadithi za kisayansi unaotokana na takwimu, uandishi wa matokeo (results-based reporting).

Pia, yanaimarisha uelewa kuhusu uhifadhi wa bayoanuai, uthabiti wa tabianchi, uhifadhi shirikishi wa jamii, na uchumi wa buluu, sambamba na kuongeza uwezo wa kutafsiri taarifa za kitaalamu kuwa maudhui yanayoeleweka kirahisi kwa wasomaji na watazamaji.
Hatua hii inalenga pia kuimarisha ushirikiano kati ya vyombo vya habari na wadau wa miradi ili kuhakikisha upo ufuatiliaji endelevu wa shughuli za uhifadhi wa mazingira ya baharini na ukanda wa pwani, hususan zile zinazofadhiliwa na Wizara ya Shirikisho la Ujerumani ya Mazingira, Uhifadhi wa Asili, Usalama wa Nyuklia na Ulinzi wa Watumiaji (BMUKN) kupitia mpango wa IKI, pamoja na mchango wa kifedha kutoka Umoja wa Ulaya (EU) nchini Tanzania.


