8.4 C
New York

Vijana na mitazamo tofauti juu ya Waziri Mkuu mpya

Published:

TOKYO, Japan
KWA mara ya kwanza katika historia ya siasa za Japan, Sanae Takaichi amekuwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi nyeti ya Waziri Mkuu.
Wakati huo huo, kama hiyo haitoshi, tafiti zinaonesha kuwa asilimia zaidi ya 74 ya waliompigia kura ni vijana wenye umri kati ya miaka 18 na 29.
Ni tofauti na Waziri Mkuu aliyepita, Shigeru Ishiba, ambaye ni asilimia 11 pekee ya vijana wenye umri wa miaka 18 hadi 29 waliokuwa wamempigia kura.
Sasa, ukiwa ni takribani mwezi mmoja umepita tangu alipoingia madarakani, vijana wa kike nchini humo wamekuwa na mitazamo tofauti juu ya Takaichi.
Ren Ichihara, ambaye ni mfanyabiashara mwenye umri wa miaka 24 mjini Tokyo, anaamini Takaichi kushika nafasi hiyo ni hatua kubwa katika harakati za wanawake kuaminiwa.
Ichihara anasema: “Naamini alichaguliwa kuwa Waziri Mkuu kutokana na uwezo wake. Alianza safari yake wakati bado jamii haiwaamini wanawake.”
Wakati huo huo, Ayano Suzuki, ambaye ana umri wa miaka 27, naye anaungana na kile anachokisema Ichihara akisema: “Kwanza, nimefurahi kuona hatimaye mwanamke anakuwa Waziri Mkuu nchini Japan.”
Kwa upande wake, Suzuki anasema Takaichi amekuwa na mvuto na ushawishi mkubwa hata kwa wananchi wasiofuatilia masuala ya siasa.
Ni kama ilivyo kwa Fumi Nakamura, mtaalamu wa lugha mwenye umri wa miaka 27, ambaye anasema: “Nimejikuta nikivutiwa tu na Takaichi …”
Hata hivyo, wakati hao wakiwa na mtazamo huo, wapo vijana wa kike, ambao hawajavutiwa na kitendo cha Takaichi kuwa Waziri Mkuu.
Miongoni mwao ni muhitimu wa Chuo Kuu mwenye umri wa miaka 27, ingawa hakutaka jina lake lianikwe. Alisema: “Watu wa aina yangu, huwa hatuvutiwi na mwanasiasa, eti kwa sababu ni mwanamke.”
Mtazamo huo unaungwa mkono na wengine, wakidai kuwa Takaichi amekuwa gumzo kutokana na jinsia yake, badala ya sera alizonazo katika kuiletea maendeleo Japan.
Lakini, wachambuzi wa siasa wanamuona Takaichi akifuata nyayo za Waziri Mkuu wa zamani, Shinzo Abe, ambaye sera zake zilijikita katika kujenga umoja wa kitaifa na kuimarisha uchumi.
Akizungumzia hilo, profesa wa tafiti wa Chuo Kikuu cha Tokyo, Sawako Shirahase, anasema: “(Takaichi) amefika hapa alipo kwa mengi aliyoiga kutoka kwa utawala wa Abe.”

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img