Na mwandishi wetu, Gazetini
KAMPUNI maarufu ya teknolojia ya Apple inakabiliwa na kashfa nzito ikitajwa kunufaika na mgogoro wa muda mrefu unaoendelea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Iko hivi; Apple imefunguliwa mashitaka ikidaiwa kunufaika kwa Siri na madini ya Cobalt, ambayo yanatajwa kuwa chanzo cha vita kati ya waasi wa M23 na Serikali ya nchi hiyo.
Jopo la wanaharakati nchini Marekani wameifikisha mahakamani Kampuni hiyo wakidai imekuwa ikitumia madini hayo kutengeneza vifaa vyake, zikiwamo simu.
Licha ya Apple kukana shutuma hizo, wanaharakati wa Marekani wanasema Apple imekuwa ikiendesha operesheni za siri kupata madini hayo.
Katika maelezo yao, kama ilivyoriootiwa na Shirika la Habari la Reuters, Apple wameyaita madai hayo kuwa ni uzushi usio na mashiko.
Lakini, kwa mujibu wa kile kilichoelezwa na wanaharakati hao, Apple Ina mtandao wa kupata madini hayo kutoka kwa vikundi vya waasi nchini DRC.
Hata hivyo, Apple haiko peke yake katika kashfa hiyo ya kunufaika na madini hayo. Pia, zipo kampuni kadhaa za China, zikiwamo Ningxia Orient, Jiujiang JinXin na Jiujiang Tanbre.
Wachunguzi wa Umoja wa Mataifa, pamoja na jumuhiya zingine za kimataifa, zimezitaja kampuni hiyo kuhusika katika uporaji wa madini kutoka DRC.
Oktoba, mwaka huu, iliibuka ripoti iliyofichua kuwa vikundi vya waasi katika maeneo ya Mashariki mwa DRC vimechota zaidi ya kilogramu 500 za dhahabu zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 70.
Aidha, taarifa ambazo Rwanda imekuwa ikikanusha mara zote ni kwamba kampuni hizo zimekuwa zikiitumia kuingia nchi jirani ya DRC na kuchukua madini kupitia vikundi vya waasi, ikiwamo M23.
M23, likitajwa kuwa ndiyo kundi kubwa zaidi la waasi, linaushikilia Mji wa Goma, ambao una utajiri wa kutisha wa madini ya Cobalt.
Kwa upande mwingine, DRC na Marekani, pamoja na Umoja wa Mataifa, zimekuwa zikiitupia lawama Serikali ya Rwanda, zikidai inashirikiana na M23.
Ni kwa muda mrefu sasa, Qatar kwa kushirikiana na Marekani zimekuwa zikionesha jitihada za kuupatia suluhisho mgogoro unaoendelea DRC.
Published:


