Na mwandishi wetu, Gazetini
TAIFA kongwe la Afrika Magharibi, Ivory Coast, limeingia katika Uchaguzi Mkuu, huku wagombea watano wakiwania kiti cha urais. Miongoni mwao ni Rais wa sasa, Alassane Ouattara.
Raia wa nchi hiyo walipiga kura Oktoba 25, mwaka huu, ikiwa ni miaka 15 tangu vurugu za baada ya Uchaguzi uliomweka madarakani kiongozi huyo.
Swali ni je, Uchaguzi wa mwaka huu utaacha simanzi ya vifo na uharibifu mkubwa wa miundombinu ulivyotokea mwaka 2010?
Kama inavyoelekeza Katiba ya nchi hiyo, endapo hakutokuwa na mgombea wa urais atakayevuka asilimia 50 ya kura, Uchaguzi utarudiwa.
Kwa upande wake, Ouattara mwenye umri wa miaka 83 anasaka muhula wake wa nne madarakani baada ya kufanya marekebisho ya Katiba mwaka 2016.
Mchumi huyo aliyewahi kufanya kazi katika Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), anatarajiwa kurejea madarakani kutokana na kazi nzuri aliyoifanya.
Chini ya utawala wake, Ivory Coast imepiga hatua kubwa kiuchumi, ikichagizwa na uwekezaji mkubwa katika miundombinu.
“Tunaingia mwaka 2025-30 tukiwa na nguvu. Maendeleo yatakuja zaidi na tuendeleza miundombinu, uzalishaji na maisha bora,” amesema Ouattara.
Hata hivyo, bado utawala wa kiongozi huyo wa Chama cha Rally of Houphouetists for Democracy and Peace (RHDP) unakumbana na upinzani mkali, wakosoaji wakieleza kutokuridhishwa na hali ya kisiasa nchini humo.
Mathalan, uamuzi wa Ouattara kubadili Katiba na kuondosha kipengele kilichokuwa kikimzuia kugombea tena ulikosolewa vikali na wachambuzi wa siasa.
Kama hiyo haitoshi, ni kitendo cha baadhi ya wanasiasa wenye ushawishi mkubwa, akiwamo Rais wa zamani, Laurent Gbagbo, kuzuiwa kugombea katika Uchaguzi wa mwaka huu.
Wengine waliowekewa kizingiti na majina yao kuondoshwa katika kinyang’anyiro ni waliowahi kuwa mawaziri wakuu, Guillaume Soro na Pascal Affi N’Guessan.
Aidha, Tidjane Thiam, ambaye ni kiongozi wa Chama cha PDCI aliyetarajiwa kumpa ushindani mkali Rais Ouattara, naye alitupwa nje ya kinyang’anyiro kwa madai ya kuwa na uraia wa nchi mbili (Ivory Coast na Ufaransa).
Kama itakumbukwa, kuondoshwa kwao kwenye mbio za kuwania urais kulisababisha maandano ya wafuasi wa vyama vikubwa viwili vya upinzani, PPA-CI na PDCI.
Kwa upande mwingine, wagombea waliopitishwa na Tume ya Uchaguzi hawaonekani kuwa na ubavu wa kukabiliana na Rais Ouattara.
Miongoni mwao ni Ahoua Don Mello, ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha African People’s Party-Cote d’Ivoire akichukua nafasi ya Gbagbo.
Mwingine ni mwanasiasa mkongwe, Simone Ehivet Gbagbo, anagombea nafasi hiyo akipeperusha bendera ya Chama cha Movement of Capable Generations (MCG).
Pia, yumo aliyekuwa Waziri wa Wanawake, Henriette Lagou Adjoua, ambaye sera zake zimejikita katika kupambania usawa wa kijinsia. “Wanawake wanapuuzwa. Nikishinda, nitahakikisha usawa wa kijinsia unakuwa kipaumbele,” amesema.
Naye mfanyabiashara maarufu, ambaye pia aliwahi kuwa waziri miaka kadhaa iliyopita, Jean-Louis Billon, anagombea nafasi ya urais.
Kupitia mikutano yake ya kampeni, ametangaza nia ya kuinua uchumi wa Ivory Coast, kutokomeza ukosefu wa ajira, kumaliza changamoto ya mfumuko wa bei, na kuipa nguvu sekta binafsi.
“Raia wa Ivory Coast wanataka mabadiliko,” amesema na kupongeza: “Tutaweza kufanikisha hilo kupitia Uchaguzi. Tuthubutu kuleta mabadiliko. Tukapige kura.”
Katika kuhakikisha Uchaguzi unafanyika pasi na kuathiri amani ya nchi hiyo, imeajiri watumishi wapya 44,000 katika vyombo vya dola, hatua ambayo hata hivyo imekosolewa ikitajwa kuwa ni mkakati wa kudhibiti wapinzani.
Jumuhiya za kimataifa, ikiwamo Amnesty International, zimekosoa hatua ya Serikali kuzuia maandano ya amani, zikiita kuwa ni uminywaji wa demokrasia, hasa kipindi hiki cha Uchaguzi.
Tayari Jumuhiya ya Uchumi kwa nchi za Ukaenda wa Afrika Magharibi (ECOWAS) imeshatua wawakilishi wake nchini Ivory Coast kufuatilia Uchaguzi huo.
Published:


