9.5 C
New York

EU, WWF watoa vifaa vya zaidi ya sh bilioni 1 kusaidia ulinzi wa misitu Tanzania

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

WIZARA ya Maliasili na Utalii imepokea jumla ya vifaa 74 vyenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni moja kwa ajili ya kuimarisha ulinzi wa misitu dhidi ya biashara holela ya mazao ya misitu.

Akizungumza Septemba 12, 2025 jijini Dar es Salaam wakati wa kupokea vifaa hivyo ambavyo vinajumuisha magari, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. Hassan Abbas, alisema vifaa hivyo vimekabidhiwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ili kuongeza nguvu katika shughuli za uhifadhi wa misitu.

Amesema vifaa hivyo vimetolewa kupitia mradi wa miaka mitatu unaoitwa Transformation of Tanzania Fuel Wood Value Chain Project 2023/26 wenye thamani ya zaidi ya Euro milioni 200 unaotarajiwa kukamilika Novemba mwakani.

“Mradi huu unalenga kuhamasisha mabadiliko chanya kutoka matumizi ya kuni kama nishati kuelekea nishati safi ili kulinda misitu dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi,” amesema Dk. Abbas.

Alibainisha kuwa mradi huo pia unalenga kuongeza uwezo wa TFS katika uhifadhi, ufuatiliaji na tathmini ya sekta ya misitu sambamba na kusaidia mikakati ya uhifadhi inayotekelezwa na halmashauri za wilaya.

Miongoni mwa vifaa vilivyokabidhiwa kupitia mradi huo ni magari ya watalii, ndege zisizo na rubani (drones), pikipiki na mifumo ya mawasiliano ya radio call kwa ajili ya ofisi za kanda za TFS kufuatilia uvunaji wa mazao ya misitu na ukusanyaji wa mapato.

Mradi huo unafadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) na kutekelezwa na serikali kwa ushirikiano na Shirika la Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF) Tanzania, Mpingo Conservation and Development Initiative na Lawyers Environmental Action Team (LEAT).

Mkurugenzi wa WWF Tanzania, Dk. Amani Ngusaru, amesema mradi huo pia unajumuisha mafunzo kwa walinzi wa misitu ngazi ya wilaya na vijiji ikiwemo maeneo ya ununuzi, ukusanyaji wa takwimu na utoaji vibali.

Aidha, alisema mifumo ya radio call itasimikwa katika kanda nne – Magharibi, Mashariki, Kaskazini na Ziwa- ambazo ndizo zinazoongoza kwa uvunaji wa mazao ya misitu.

Aliongeza kuwa utekelezaji wa mradi huo unahusisha mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Tanga, Pwani, Mwanza na Tabora kwa kuwa ndizo zinazoongoza kwa uzalishaji na matumizi ya kuni kama nishati.

Kwa upande wake Kamishna wa Uhifadhi, Prof. Dos Santos Silayo, alisema vifaa vingine vilivyokabidhiwa ni mashine za malipo kwa kadi (POS) pamoja na boti za doria.

Alishukuru Umoja wa Ulaya kwa kufadhili mradi huo akisema: “Tutavitumia vifaa hivi kwa ufanisi ili kuhakikisha biashara ya mazao ya misitu inafanyika kwa uwajibikaji na kwa kuzingatia misingi ya uhifadhi.”

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img