LONDON, Uingereza
FAINALI za Kombe la Dunia za mwaka huu ziko njiani. Zitaanza Juni 11 na kufanyika kwa mwezi mmoja hadi Julai 19, 2026, huku mechi ya ufunguzi ikizikutanisha Mexico na Afrika Kusini.
Timu ya Taifa ya England ‘Three Lions’ ni miongoni mwa zile zinazopewa nafasi ya kutwaa ubingwa wa mashindano hayo makubwa zaidi katika ulimwengu wa kandanda.
England haibeba ‘ndoo’ ya michuano hiyo tangu mwaka 1966 lakini safari hii timu hoyo inaweza kutimiza ndoto chini ya kocha raia wa Ujerumani, Thomas Tuchel.
UZOEFU WA KOCHA WAKE
Tuchel ni mmoja ya makocha bora na wenye uzoefu wa kutosha. Ametwaa mataji mengi akiwa na Borussia Dortmund, Bayern Munich na PSG.
Kama hiyo haitoshi, aliipa Chelsea taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na Chelsea msimu wa 2020-21, akiifunga Manchester City ya Pep Guardiola bao 1-0 katika mchezo wa fainali.
KIWANGO CHA TIMU
England imekuwa na ubora wa hali ya juu kwa miaka ya hivi karibuni. Ilifuzu fainali za mwaka huu ikiwa kileleni mwa Kundi K baada ya kushinda mechi zote nane.
Pia, kama haijasahaulika, Three Lions ilikata tiketi ikiwa haijaruhusu bao, huku ikifunga mabao 22 katika mechi nane hizo.
UBORA WA KIKOSI
Ukiacha mastaa Harry Kane, Bukayo Saka, Phil Foden, Cole Palmer, Declan Rice, Morgan Rogers, Morgan Gibbs-White na Jude Bellingham, England ina makinda wanaofanya vizuri katika soka la Ulaya kwa sasa.
Unaweza kuwatolea mfano Elliot Anderson, Kobbie Mainoo na Adam Wharton, ambao ni viungo wanaowika Ligi Kuu ya England msimu huu. Ni kikosi chenye mchanganyiko wa wazoefu na ‘damu changa’.
UWEPO WA KANE
Kwa mashabiki wa England, tumaini lao kwenye safi ya ushambuliaji lipo kwa nahodha wao anayekipiga Bundesliga akiwa na Bayern Munich, Harry Kane.
Kane, mfungaji bora wa Kombe la Dunia mwaka 2018 nchini Urusi, amekuwa kwenye kiwango bora msimu huu wa 2025-26, akifunga mabao 58 na kutoa ‘asisti’ nane katika mechi 54 alizoshuka dimbani.


