11.6 C
New York

Upinzani Burundi watishia kutoshiriki uchaguzi wa rais

Published:

BUJUMBURA, Burundi

MVUTANO wa kisiasa umeanza kuongezeka nchini Burundi baada ya vyama vikuu vya upinzani kutangaza kusitisha ushiriki wao katika uchaguzi wa rais wa mwaka 2027 hadi pale mazungumzo ya kitaifa yatakapofanyika.

Hatua hiyo imekuja baada ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (CENI) kutangaza rasmi kuwa uchaguzi wa urais utafanyika Mei 3, 2027.

Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa Ijumaa, vyama vya upinzani vya CNL, UPRONA, CODEBU, DCP na FRODEBU vimesema haviwezi kushiriki katika uchaguzi huo bila kuwepo kwa mageuzi ya kisiasa na uhakikisho wa uchaguzi huru na wa haki.

Vyama hivyo vimedai kuwa bado vina kumbukumbu mbaya ya uchaguzi wa wabunge wa mwaka 2025, uliokumbwa na malalamiko ya ukiukwaji wa taratibu na kasoro mbalimbali za uchaguzi.

Katibu Mkuu wa chama cha UPRONA, Olivier Nkurunziza, amesema iwapo uchaguzi wa 2027 utaendeshwa kwa mfumo uleule wa mwaka 2025, kushiriki kwake kutakuwa ni “kuhalalisha uchaguzi usio na haki.”

“Ikiwa uchaguzi utaandaliwa kama tulivyoona mwaka 2025, kushiriki itakuwa ni uwongo. Hali hiyo inaweza kuongeza migogoro katika mshikamano wa kijamii,” amesema Nkurunziza.

Aidha, amedai kuwa CENI bado haijajitegemea kikamilifu kisiasa, hivyo kuna haja ya kuwepo kwa mazungumzo ya kitaifa yatakayohakikisha taasisi hiyo inafanya kazi kwa uhuru.

Kauli hiyo imekosolewa vikali na chama tawala cha CNDD-FDD. Katibu wa mawasiliano wa chama hicho, Doriane Munezero, amesema vitisho vya kususia uchaguzi vinadhoofisha demokrasia ya Burundi.

“Ni jambo la kusikitisha kuona kila uchaguzi ukikaribia baadhi ya vyama vinaweka masharti ya kushiriki. Demokrasia haiwezi kujengwa kwa vitisho vya kususia uchaguzi,” amesema Munezero.

Hadi sasa, Serikali ya Burundi haijatoa msimamo rasmi kuhusu ombi hilo la mazungumzo ya kitaifa. Hata hivyo, chama tawala tayari kimemtangaza Évariste Ndayishimiye kuwa mgombea wake wa urais katika uchaguzi huo.

Mwaka 2025, mmoja wa viongozi maarufu wa upinzani nchini humo, Agathon Rwasa, alizuiwa na CENI kugombea ubunge, hatua iliyozua malalamiko makubwa kutoka kwa makundi ya upinzani.

Kadri uchaguzi wa 2027 unavyokaribia, hali ya kisiasa nchini Burundi inaendelea kuwa tete huku kukiwa na hofu ya kuongezeka kwa mvutano kati ya Serikali na vyama vya upinzani.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img