LONDON, Uingereza
NI takribani mwezi mmoja umebaki kabla ya kuanza kwa fainali za Kombe la Dunia za mwaka huu. Michuano hiyo itaanza Juni 11, 2026, ikifanyika katika nchi tatu (Mexico, Marekani na Canada).
Je, Argentina itatetea ubingwa wake iliouchukua katika fainali zilizopita za mwaka 2022 nchini Qatar? Makala haya yanaangazia mambo makubwa matano kuhusu fainali hizo.
NANI KUTWAA UBINGWA?
Kwa sasa, mataifa nane ndiyo yanayopewa nafasi kubwa. Ni Brazil, Ujerumani, Argentina, Ufaransa, Uruguay, Hispania na England.
Brazil, mabingwa mara tano, hawajabeba taji hilo tangu mwaka 2002, wakati England Ina miaka 60 bila ‘ndoo’ ya michuano hiyo.
Hata hivyo, Ureno na Ubelgiji, pamoja na Uholanzi, nazo zinaweza kufanya lolote wakati wa fainali hizo.
WENYEJI KUFANYA MAAJABU?
Historia inaonesha kuwa wenyeji wamekuwa na faida kubwa. Mwaka 1998, Ufaransa ilitwaa ubingwa wake wa kwanza ikiwa mwenyeji. Miaka minne baadaye, Korea Kusini walifika nusu fainali wakiwa wenyeji.
Marekani, baada ya kukosekana mwaka 2018, ilirejea kwenye fainali za mwaka 2022 na kufika hatua ya 16 Bora.
Mexico, kwa upande wao, hii ni mara ya tatu kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia baada ya kufanya hivyo mwaka 1970 na 1986. Historia inaonesha kuwa Mexico imekuwa ikiishia hatua ya 16 Bora tangu mwaka 1994.
MESSI V RONALDO: NANI KUCHEKA, NANI KULIA?
Lionel Messi atavaa kitambaa chake cha unahodha kuiongoza Argentina. Atakuwa amefikisha umri wa miaka 39.
Messi alisema angestaafu baada ya fainali za mwaka 2022 nchini Qatar, lakini alibadili ‘gia angani’ waliponyakua ubingwa wao wa kwanza tangu mwaka 1986.
Mpinzani wake, Cristiano Ronaldo, naye ndiye nahodha wa timu ya taifa ya Ureno chini ya kocha raia wa Ubelgiji, Roberto Martinez.
Ronaldo ana mataji na tuzo nyingi. Anashikilia rekodi nyingi, ikiwamo ya mchezaji mwenye mabao mengi katika historia ya timu za taifa. Kombe la Dunia ndiyo taji pekee analokosa kwenye kabati lake.
YAMAL, HAALAND KITAWAKA SANA
Lamine Yamal ameanza kufananishwa na Messi kutokana na uwezo wa uwanjani na historia yake ya kuibuliwa na ‘academy’ ya Barcelona.
Yamal (18), aliiongoza Hispania kutwaa ubingwa wa fainali za EURO mwaka 2024, akifunga bao lililowavusha hatua ya nusu fainali.
Haaland, kwa upande wake, ana umri wa miaka 25. Achana na rekodi zake akiwa na Man City, amefunga mabao 55 katika mechi 49 tu alizocheza timu ya taifa ya Norway.
WAGENI NAO VIPI?
Oktoba, 2025, Cape Verde iliandika historia ya kuwa taifa dogo zaidi (watu 525,000) kukata tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia.
Mwezi mmoja baadaye, rekodi hiyo ilivunjwa baada ya Kisiwa cha Curacao chenye watu 155,000 nacho kufuzu michuano hiyo. Mataifa mengine yakayoshiriki kwa mara ya kwanza ni Jordan na Uzbekistan.
DRC, IRAQ NDANI YA NYUMBA
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imerejea Kombe la Dunia baada ya kuikosa michuano hiyo tangu mwaka 1974.
Iraq nayo imerudi baada ya miaka 40 ya kuwa nje. Mataifa mengine ni Scotland, Norway na Austria, kila moja ikiwa imekosa ushiriki kwa miaka 28.
Kwa upande mwingine, Uturuki nayo itashiriki kwa mara ya kwanza tangu ilipofika nusu fainali katika michuano ya mwaka 2002.


