Na mwandishi wetu, Gazetini
MIAKA 65 iliyopita, mataifa 14 ya Afrika yalipata uhuru kutoka kwa Ufaransa. Je, ni kwa kiasi gani yamepiga hatua tangu mwaka 1960?
Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UN), mataifa nane kati ya 14, bado yanasota katika nafasi za chini za viwango vya umasikini duniani. Miongoni mwao ni Chad, Mali, Burkina Faso na Niger.
Matthias Basedau ambaye ni Mkurugenzi wa Taasisi inayojihusisha na masuala ya Afrika (GIGA), anazitaja sababu ya umasikini kwa mataifa hayo kuwa ni kukosa ardhi zenye rutuba kwa ajili ya kilimo, idadi kubwa ya watu, na migogoro ya kisiasa.
Kubwa ni migogoro ya kisiasa. Basedau anazitolea mfano Mali, Burkina Faso na Niger, ambazo siasa zake zimegubikwa na mapinduzi ya kijeshi katika miaka ya hivi karibuni.
Pia, viongozi kung’ang’ania madarakani ni tatizo jingine kwenye siasa za mataifa hayo. Rais wa Ivory Coast, Ouattara, ana umri wa miaka 83 lakini bado ametangaza kuwania katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Iko hivyo pia kwa mwenzake wa Cameroon, Paul Biya, ambaye atagombea katika Uchaguzi ujao, licha ya umri wake wa miaka 92. Ni kama ilivyo kwa Rais wa Togo, Faure Gnassingbe, ambaye anataka kubaki madarakani bila kufanyika kwa Uchaguzi.
Kwa upande mwingine, licha ya kuzikabidhi uhuru miaka 65 iliyopita, bado Ufaransa imeendelea ‘kuyaweka mfukoni’ makoloni yake. Hiyo ni pamoja na kuwa na kambi za kijeshi katika mataifa hayo.
Mfano wa kambi hizo ni ile iliyoko Djibouti, ingawa Serikali za Chad, Senegal na Ivory Coast zimefanikiwa kuziondosha, ingawa bado Ufaransa inashikilia sekta muhimu katika mataifa hayo. Mfano mzuri ni sekta ya fedha na ile ya mawasiliano.
Published:


