Na mwandishi wetu, Gazetini
HATUA ya wawakilishi wa M23 kutohudhuria mkutano wa kusaini mkataba wa amani kati yake na Serikali umeibua hofu, wengi wakiamini bado kuna safari ndefu ya kurejesha amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Pande mbili hizo zilipaswa kukutana Agosti 18, mwaka huu, mjini Doha, Qatar, baada ya mkataba wa awali wa Julai 19, ambapo zilikubaliana kusitisha mapigano.
Hata hivyo, kitendo cha M23 kutokutuma wawakilishi katika mkutano wao wa Doha mapema wiki hii ni kama kinakwamisha jitihada za kumaliza mgogoro wa muda mrefu kati ya pande hizo.
Katika taarifa yao baada ya kutohudhuria, M23 wameishutumu Serikali ya DRC kwa kukiuka baadhi ya makubaliano ya Julai 19, ikiwamo kutokuwaachia wapiganaji wao wanaoshikiliwa gerezani.
M23, kwa upande wao, nao wanalaumiwa kwa kuendeleza mauaji, kama inavyoelezwa na ripoti ya Taasisi ya Haki za Binadamu ya Amnesty, kwamba Kundi hilo limeua watu takribani 140 kwa kipindi cha Julai pekee.
Ikumbukwe, M23 imeendelea kuwa na nguvu kubwa nchini DRC, ambapo inatawala majimbo mawili ya ya Kaskazini na Kusini mwa Kivu.
Kwa wachambuzi wa siasa barani Afrika, chanzo kikubwa cha M23 na Serikali ya DRC kushindwa kufikia makubaliano ni kila upande kutokubaliana na mwingine katika baadhi ya mambo.
Akitolea mfano, Nkere Ntanda, ambaye ni mtaalamu wa sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha Kinshasa, anasema: “Hakuna upande ulio tayari kukubaliana na matakwa ya mwingine.”
Ntanda anasema wakati Serikali ya DRC ikitaka kufutika kabisa kwa M23, Kundi hilo linataka kuhakikishiwa nafasi katika siasa za nchi hiyo hata baada ya mgogoro kumalizika.
Kwa upande mwingine, wachambuzi wanaiona hatari kubwa endapo pande mbili hizo zitaendelea kuvutana katika meza ya mazungumzo na kushindwa kupata suluhisho la mgogoro huo.
Reagen Miviri, ambaye ni msomi wa masuala ya migogoro katika Chuo cha Ebuteli nchini DRC, anasema: “Umakini inahitajika. Vinginevyo, hali inaweza kuwa mbaya zaidi.”
Kwa nyakati tofauti, viongozi wenye ushawishi mkubwa katika siasa za Afrika, akiwamo Rais wa zamani wa Nigeria, Olusegun Obasanjo, wamejaribu bila mafanikio kumaliza uhasimu uliopo kati ya M23 na Serikali ya DRC.
Lakini, mchambuzi Ntanda anaamini mataifa yenye nguvu kubwa ya kiuchumi, akitolea mfano Marekani na Qatar, yana nafasi kubwa ya kumaliza mgogoro huo uliosabahisha maelfu ya wananchi wa DRC kukimbia makazi yao.
Marekani, licha ya kwamba ni mshirika mkubwa wa Rwanda, imekuwa ikiinyooshea kidole nchi hiyo kwa madai kuwa imekuwa ikiwaunga mkono wapiganaji wa M23.
Je, kufikia makubaliano ya M23 kutarejesha amani iliyopotea DRC? Jibu ni hapana, kwa mujibu wa wachambuzi wa siasa wa ndani na nje ya Taifa hilo.
“Bado kuna nguvu kubwa inahitajika. M23 ni moja tu kati ya vikundi vya waasi takribani 100 vilivyofanya mashambulizi Mashariki mwa DRC,” anasema Ntanda.
Ntanda anatolea mfano wapiganaji wa ADF wanaojinasibisha na Dini ya Uislam, taarifa zikieleza kuwa wanashirikiana na Kundi maarufu la ugaidi la IS.
Ripoti ya Umoja wa Mataifa (UN) kupitia Baraza lake la Usalama inaeleza kuwa Kundi hilo la ADF limesababisha vifo vya watu takribani 52 katika miji ya Beni na Lubero.
Published:


