8.4 C
New York

Kucha za bandia, ‘make-up’ chanzo ugonjwa wa pumu

Published:

LONDON, England
UMAKINI unahitajika. Utafiti umeonesha kuwa kucha bandia ni chanzo kikubwa cha ugonjwa wa pumu, licha ya wanawake wengi, hasa wa maeneo ya mjini, kuziona ni urembo.
Hiyo ni kwa mujibu wa utafiti wa Taasisi ya magonjwa ya Moyo, Mapafu na Damu ya Marekani, ambao ulihusisha watu takribani 40,000.
Wakati huo huo, mbali ya kucha, pia urembo wa midomo (lipstick) nao umetajwa kuwa na uhusiano wa karibu na ugonjwa huo wa pumu.
Pumu (asthma) ni ugonjwa unaoathiri mfumo wa hewa katika mapafu, ukitajwa kuwatesa watu zaidi ya milioni 5 nchini Uingereza.
Huku dalili zake zikiwa ni kukooa mara kwa mara, pia upumuaji wa shida, kwa kuzitaja kwa uchache, ripoti ya Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) inaeleza kuwa ni ugonjwa unaoathiri watu zaidi ya milioni 230.
Utafiti huo uliochapishwa katika jarida la Environment International, umetokana na takwimu zilizokusanywa kwa miaka 12, ukihusisha pia bidhaa za urembo 41.
Sasa, majibu yake yameonesha kuwa matumizi ya kucha za bandia, rangi za midomo (lipstick) na urembo wa uso (make-up) yanaongeza hatari ya kupata ugonjwa wa pumu kwa asilimia 18.
Katika wanawake wanaotumia kucha za bandia, lipstick au make-up, asilimia 45 walibainika kupata ugonjwa wa pumu ya ukubwani.
Ni tofauti kidogo na tafiti za awali, ambazo zilionesha kuwa utumiaji wa bidhaa hizo za urembo kwa mjamzito unasababisha ugonjwa wa pumu kwa mtoto aliye tumboni.
Aidha, utafiti huo unaeleza kuwa walio hatarini zaidi ni wale wanaotumia vitu hivyo mara tano kwa wiki.
Hata hivyo, wataalamu wa Taasisi hiyo wanakiri kuwa utafiti wao haukubaini aina ya bidhaa zilizo hatari zaidi, ingawa wanaonya kuwa kemikali zinazotumika zinaathiri mfumo wa upumuaji katika mapafu.
Baadhi ya kemikali hizo, zikiwamo PFA, kwa mujibu wa utafiti, zinadhohofisha mfumo wa kinga- miwili wa mtumiaji.
“Majibu ya utafiti wetu yanachochea uhitaji wa mtu kuwa makini na bidhaa anazotumia,” inaeleza ripoti ya utafiti huo.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img