MOSCOW, Urusi
MAWAZIRI wa Mambo ya Nje wa Urusi na China wamezungumzia uwezekano wa kumaliza vita inayoendelea kati ya Taifa hilo la Ulaya na majirani zao, Ukraine.
Pia, katika mazungumzo hayo, Mawaziri hao waligusia uhusiano usio na afya kati ya mataifa yao na Marekani.
Waziri wa Urusi, Sergei Lavrov, na mwenzake wa China, Wang Yi, walifanya mazungumzo hayo leo Jumapili mjini Beijing.
“Pande mbili zilizungumzia uhusiano wao na Marekani, pia namna ya kumaliza mgogoro wa Ukraine,” ilieleza taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi.
Vilevile, taarifa ilieleza kuwa viongozi hao walijadili namna ya mataifa hayo yanavyoweza kushirikiana katika masuala ya kimataifa.
Marekani imekuwa ikiiona China kuwa ni mpinzani wake mkubwa wa kiuchumi, huku ikiitazama Urusi kwa jicho la tishio.
Mwanzoni mwa mwaka 2022, Urusi na China zilitangaza kuwa zina ‘urafiki usio na mipaka’ baada ya Rais Vladmir Putin kutembelea Beijing.
Wakati mwingine, Rais Putin amekuwa akiitaja wazi kuwa China ni mshirika wao mkubwa katika masuala mbalimbali.
Published:


