NAIROBI, Kenya
WAKATI maandamano ya raia wanaoipinga Serikali yakiendelea, Rais wa Kenya, William Ruto, ameagiza waandamanaji wapigwe risasi za miguu.
Agizo hilo linakuja wakati huu jumuhiya za kimataifa zikilaani nguvu kubwa inayotumiwa na polisi kudhibiti maandamano hayo.
Kufikia Jumatatu ya wiki hii, ilisharipotiwa kuwa watu 31 wameshapoteza maisha.
Hata hivyo, licha ya kusema hataki kuona raia wakiuawa, Rais Ruto aliwaagiza polisi kuwapiga risasi za miguu waandamanaji watakaofanya uharibifu.
“Yeyote atakayekutwa akichoma biashara au mali za mtu, apigwe risasi mguu, apelekwe hospitali kisha baadaye afunguliwe mashitaka, hakikisheni mnavunja miguu,” alisema Ruto.
“Chini ya uongozi wangu, Kenya haiwezi na haitaongozwa kwa vitisho, ugaidi, au vurugu.”
Mbali ya vifo 31, watu zaidi ya 100 wameshajeruhiwa katika maandamano yanayoendelea.
Kwa upande wa Umoja wa Mataifa (UN), taarifa yake imekemea nguvu kubwa wanayotumia polisi dhidi ya waandamanaji.
Published:


