18 C
New York

Utafiti: Uvutaji wa bangi chanzo ugumba kwa wanawake

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini
UTAFITI nchini Canada umebaini kuwa wanawake wanaojihusisha na utumizi wa dawa za kulevya aina ya bangi wako hatarini kupata tatizo la kushindwa kushika ujauzito (ugumba).
Matokeo hayo ni kwa mujibu wa utafiti wa Taasisi ya magonjwa ya uzazi ya CReATe Fertility Centre, kwa kushirikiana na wanasayansi wa Chuo Kikuu cha Toronto.
Ukihusisha wanawake 1,059, wataalamu waliosimamia utafiti huo walibaini kuwa bangi ina madhara ya moja kwa moja katika mchakato mzima wa yai la mwanamke kukutana na mbegu za mwanaume.
Kwa mujibu wa utafiti, zoezi la mbegu kurutubisha yai ili kuzalisha ujauzito huathiriwa, hivyo kuwa ngumu kwa mwanamke anayevuta bangi kushika ujauzito.
Hata hivyo, wataalamu wa afya nchini Ujerumani wamezungumzia utafiti huo wakisema bado haujaeleza kwa kina juu ya uhusiano wa bangi na ugumba kwa wanawake.
Dkt. Artur Mayerhofer, ambaye ni mmoja ya madaktari bingwa kutoka Chuo Kikuu cha Ludwig Maximilian University (LMU) cha mjini Munich, ametoa maoni yake akisema:
“Ni utafiti mzuri, lakini haujaonesha tofauti ya madhara kati ya watumiaji wa umri mmoja na mwingine. Suala la kushika ujauzito pia huwa na uwezekano mdogo kila umri wa mwanamke unapoongezeka,” anasema Dkt. Mayerhofer.
Kwa upande wake, msomi mwingine, Dkt. Wolfgang Paulus anaukosoa utafiti wa Canada akisema haujaeleza kiwango cha utumizi wa bangi kinachoweza kumsababishia mwanamke tatizo la ugumba.
Wakati huo huo, Dkt. Paulus anaongeza: “Changamoto kubwa ya utafiti huo ni kutokuweka wazi; je, ni kwa kiasi gani cha matumizi ya bangi, mwanamke atakuwa ameathirika?”

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img