LOME, Togo
MIEZI mitatu iliyopita, siasa za Taifa la Togo zilitikiswa na hatua ya Rais Faure Gnassingbe kutangaza kujiuzulu. Tangu hapo, wadhifa huo umekuwa chini ya Jean-Lucien Savi de Tove.
Hata hivyo, licha ya kutangaza kujiweka kando, Gnassingbe analalamikiwa kwa kile kinachotajwa kuwa ni kuendelea kuiongoza Togo, huku Rais wa sasa, Savi de Tove, akibaki kama kivuli tu.
Kwa sasa, Gnassingbe ni Rais wa Baraza la Mawaziri, nafasi ambayo haikuwepo, bali imeanzishwa baada ya mabadiliko ya Katiba.
Nafasi hiyo, kwa mujibu wa wachambuzi wa siasa, Gnassingbe ana mamlaka yote aliyokuwa nayo akiwa kwenye kiti cha urais.
Wakosoaji wake, wakiwamo wanasiasa wa upinzani na wanaharakati wa haki za binadamu, wameyafananisha mazingira hayo na ‘utekaji wa Katiba’.
Si tu mamlaka makubwa aliyonayo, bali pia nafasi hiyo si ya kuchaguliwa kwa kupigiwa kura na wananchi, bali Gnassingbe aliipata kwa kupitishwa na Bunge, ambalo limejaa wanachama wa Chama chake cha UNIR (Union for the Republic).
Wakati huo huo, kile kinacholalamikiwa zaidi na wakosoaji wake ni kwamba nafasi hiyo haina ukomo, hivyo Gnassingbe anaweza kuishikilia hadi pale atakapoamua kuachia.
Kwa upande wao, wananchi wa Togo nao hawakubaliani na kinachoendelea. Maandamano yao ya kutaka Serikali ijiuzulu, ambayo yalisababisha vifo vya watu saba, yanathibitisha hilo.
FAMILIA INAYOTAWALA KWA MIAKA 50
Ifahamike kuwa familia ya Gnassingbe imeiongoza Togo kwa miaka 58 sasa na inashikilia nafasi nyingi nyeti katika Serikali ya nchi hiyo ya Afrika Magharibi.
Gnassingbe, kwa upande wake, alikuwa Rais wa Togo tangu mwaka 2005, alipochukua nafasi hiyo kutoka kwa baba yake, Gnassingbe Eyadema, ambaye aliiongoza nchi hiyo kwa miaka zaidi ya 40.
“Ukweli ni kwamba hili ni tatizo kubwa. Hata maandamano yaliyotokea nchini (Togo) hivi karibuni hayakutokana tu na matukio ya watu kukamatwa na polisi mara kwa mara, bali pia yalitokana na kuchoshwa na kitendo cha familia hii kuongoza kwa miaka zaidi ya 50,” anasema Pape Ibrahima Kane, ambaye ni Mkurugenzi wa Taasisi ya demokrasia ya Open Society Initiative.
Akizungumzia nafasi aliyonayo Gnassingbe kwa sasa, ambayo mamlaka yake hayatofautiani na aliyokuwa nayo akiwa rais, Kane anasema Serikali ya Togo imekiuka Mkataba wa Demokrasia, Uchaguzi na Utawala uliosainiwa na wanachama wa Umoja wa Afrika (AU), ikiwamo Togo, mwaka 2007.
“Mkataba huo ulizitaka nchi zote kuwa na chaguzi huru na haki, pia kuhakikisha zinakuwa na serikali zinazoheshimu uwakilishi wa wananchi na misingi ya demokrasia,” anasema.
HISTORIA MPYA KUANDIKWA?
Lakini sasa, wachambuzi wa siasa wanahofia kuwa huenda Gnassingbe anakuwa kiongozi wa kwanza barani Afrika kujitengenezea mazingira ya kubaki madarakani kwa muda mrefu bila kupigiwa kura na wananchi.
Kwamba walau baadhi ya marais, akiwamo Yoweri Museveni wa Uganda, walibadili Katiba ili wagombee tena nafasi hiyo, lakini siyo Gnassingbe ambaye sasa hatohitaji kupigiwa kura na wananchi.
“Hii inaweza kuwashawishi viongozi wengine kubadili Katiba kwa mfumo huo,” anasema mwanasheria wa haki za binadamu nchini Togo, Esso-Dong Divin Yamard Kong.
JESHI KUPINDUA SERIKALI?
Kuanzia mwaka 2020 hadi 2023, yamekuwapo matukio sita ya jeshi kupindua serikali katika nchi za Magharibi mwa Afrika. Mathalan, ilikuwa hivyo nchini Mali na Burkina Faso.
Wachambuzi wanaonya kuwa huenda sasa ikawa ni zamu ya Togo, Uganda na Guinea, ambako viongozi wameonesha nia ya kutokutaka kuachia kiti cha urais.
Hata hivyo, wachambuzi wanaitolea mfano Mali, wakisema mfumo wa jeshi kuongoza Serikali unawanyima raia wa kigeni haki ya kuchagua kiongozi wanayemtaka.
Pia, kumekuwapo na utamaduni wa viongozi wa kijeshi kung’ang’ania Ikulu baada ya kupindua serikali zao. Hilo lilitokea nchini Mali mwaka huu, ambapo kiongozi wa kijeshi, Assimi Goita, alijiongezea miaka mitano ya kubaki madarakani.
KUNA NINI IKULU?
Museveni mwenye umri wa miaka 80, ametangaza kuwa atagombea kwa awamu ya saba kiti cha urais katika Uchaguzi Mkuu ujao. Ni baada ya kuifanyia mabadiliko Katiba ya nchi hiyo na kuondoa kigezo cha umri.
Rais wa Jamhuri ya Kati, Faustin Archange Touadera, naye ametangaza kugombea wa awamu ya tatu. Paul Biya wa Cameroon anataka awamu ya nane madarakani, licha ya umri wake wa miaka 92.
Denis Sassou-Nguesso waJamhuri ya Congo ameliongoza Taifa hilo kwa miaka 41. Mwenzake wa Ivory Coast, Alassane Ouattara, ana umri wa miaka 83 na ametangaza nia kuelekea Uchaguzi ujao wa Oktoba, mwaka huu.
Vipi kuhusu Teodoro Obiang Nguema wa Guinea ya Ikweta? Nguema ndiye rais aliyedumu madarakani kwa muda mrefu zaidi duniani. Ana umri wa miaka 83 na ameiongoza Guinea tangu mwaka 1979.
Published:


