13.9 C
New York

Awashitaki wazazi kisa kumzaa bila ridhaa yake

Published:

NEW DELHI, India

INAWEZA kukushangaza kidogo. Huenda pia ikakufikirisha, achilia mbali kuhisi ni simulizi ya kuikirika tu. La hasha! Ni kisa cha kweli kabisa.

Kijana raia wa India, Raphael Samuel, amewashangaza wengi kwa kitendo chake cha kuwafungulia mashitaka wazazi wake.

Kisa? Samuel, mkazi wa Mumbai mwenye umri wa miaka 27, amewashitaka wazee wake hao kwa kile alichodai kuwa walimzaa bila kukubaliana naye.

Kwa mujibu wa kile alichokieleza Samuel kuliambia Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), haukuwa uamuzi wake kuzaliwa na wazazi hao.

Akisisitiza hilo, Samuel aliiambia BBC kuwa wazazi hukutana kwa starehe zao, hivyo mtoto anapozaliwa huwa amekosa haki ya kuchagua aina ya familia anayotaka kuzaliwa.

Ni kwa maana hiyo basi, Samuel anaamini wazazi wanapaswa kumlipa fedha mtoto wao kwa kipindi chote cha maisha yake kwa kuwa walimlazimisha kuwa kwenye familia yao.

Anasema alianza kupata wazo hilo tangu akiwa na umri wa miaka mitano tu, baada ya baba yake kukosa jibu alipomuuliza sababu ya kumleta duniani.

Sasa, baada ya Samuel kuibuka na madai hayo, mama yake, Kavita Karnad, ambaye ni mwanasheria kama ilivyo kwa mumewe, anaongeza kuwa anasubiri kuona mwenendo wa kesi hiyo.

“Nasubiri kuona mtoto wangu akiwapeleka mahakamani wazazi wake, akifahamu wazi kuwa sisi sote ni wanasheria.

“Kama Samuel atakuja na hoja ya msingi juu ya hili la kutaka ridhaa ya kuzaliwa, nitakiri kosa langu,” anasema Kavita.

Lakini, mama huyo anakiri kuvutiwa mno na ubunifu wa mawazo aliokuja nao mtoto wao. “Nimefurahi kuona kijana wangu hahofii, ana mawazo ya kipekee. Naamini anatafuta njia ya kuwa huru na mwenye furaha.”

Msingi wa hoja ya Samuel ni falsafa inayofahamika kwa jina la ‘anti-natalism’, ambayo inapingana na utamaduni wa asili wa binadamu kuzaliana.

Waumini wa falsafa hiyo wanatolea mfano mtoto aliyerithi magonjwa kutoka kwa wazazi wake. Pia, wanatolea mfano mtoto aliyezaliwa katika umasikini.

Wanaamini hatokuwa ametendewa haki na huenda asingekubali kuwa sehemu ya familia hiyo endapo angepewa haki ya kuulizwa kabla ya kuzaliwa.

Hata hivyo, Samuel anakiri kukumbana na ukosolewaji mkubwa tangu alipotangaza nia yake ya kuwashitaki wazazi.

Hasa katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook, wengi wameonekana kumshambulia, achana na kutokukubaliana naye.

“Wanaonibeza, acha tu waendelee kunibeza lakini nimeona wengi wakiniubga mkono, ingawa hawawezi kujitokeza hadharani,” anasema.

Miongoni mwao, wanamdhihaki Samuel na kusema anatafuta umaarufu tu. “Sio kama natafuta umaarufu, ila nataka wazo langu liende mbali. Ni rahisi tu, kwamba siyo lazima uwe na mtoto,” anasisitiza.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img