Na Faraja Masinde, Gazetini
Serikali imeshauriwa kuchukua hatua madhubuti ikiwamo kutoa elimu kwa wananchi na kuweka alama za kudumu katika maeneo yenye mapitio ya wanayama (shoroba) ili kupunguza madhara yatokanayo na muingiliano wa binadamu na wanyamapori.
Ushauri huo umetolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasi na Utalii kupitia taarifa yake iliyowasilishwa mapema mwezi huu Bungeni jijini Dodoma.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Ally Juma Makoa amekiri kuwa kuna changamoto za kuzibwa kwa shoroba katika Hifadhi za Taifa.
“Serikali itoe elimu kwa wananchi kuhusu maeneo ya shoroba za wanyamapori ili kupunguza muingiliano kwa wanyama na binadamu unaoleta athari kwa pande zote.
“Maeneo ya hifadhi na mifumo ikolojia ya wanyamapori yanaunganishwa na shoroba ambazo huruhusu wanyamapori kuhama kutoka hifadhi au eneo moja kwenda nyingine kwa malengo mbalimbali ikiwemo kujihami, kuzaliana, maeneo ya mtawanyiko na maeneo muhimu kwa ajili ya kupata chakula na maji wakati wa msimu kiangazi wa mwaka.
“Kamati inaipongeza Wizara kwa kushirikiana na wadau wa uhifadhi nchini, hususan Shirika la Misaada la Watu wa Marekani (USAID) kupitia mradi wa 19 RTI – Tuhifadhi Maliasili kuweza kufanya tathmini na kubainisha shoroba 61 za wanyamapori nchini na kuandaa Mpango kazi wa vipaumbele wa kuongoa shoroba hizo na kuandaa mwongozo wa utekelezaji wa mpango kazi huo,”
Makoa
“Kamati inaipongeza Wizara kwa kushirikiana na wadau wa uhifadhi nchini, hususan Shirika la Misaada la Watu wa Marekani (USAID) kupitia mradi wa 19 RTI – Tuhifadhi Maliasili kuweza kufanya tathmini na kubainisha shoroba 61 za wanyamapori nchini na kuandaa Mpango kazi wa vipaumbele wa kuongoa shoroba hizo na kuandaa mwongozo wa utekelezaji wa mpango kazi huo,” amesema Makoa na kuongeza kuwa:
“Kuziba kwa shoroba hizi kumepelekea changamoto nyingi hususan migongano baina ya binadamu na wanyamapori inayosababishwa na Wananchi wanaoendesha shughuli zao za kijamiii na kiuchumi katika maeneo ya shoroba ambapo wanakabiliwa na athari za kujeruhiwa; kuuawa; mazao kuharibiwa na mifugo kuuawa na hivyo kuongeza kiwango cha umaskini kwa wananchi; na wanyamapori kushindwa kubadilishana vinasaba (genetic exchange) na hivyo kusababisha kupotea kwa vizazi kwa baadhi ya wanyamapori ambao hawaruhusu inbreed,” amesema Makoa.
Amesema umefika wakati kwa serikali kuweka alama za kudumu kwenye maeneo yanliainishwa kama shoroba.
“Ni wakati sasa wa Serikali kuweka alama za kudumu kwenye maeneo yaliyoanishwa kama shoroba ili kudhibiti uvamizi wa shughuli za kibinadamu,” amesema Makoa.
Hali ya shoroba
Akizungumza hivi kari buni mjini Bagamoyo mkoani Pwani, Meneja Ushirikishwaji wa Sekta Binafsi wa Mradi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) wa Tuhifadhi Maliasili, Dk. Elikana Kalumanga alibainisha kuwa shoroba zimekuwa zikiathiriwa na shughuli za binadamu hususan kilimo na kuhatarisha uwepo wa maeneo hayo na maisha ya wanyamapori kwa ujumla.
“Shoroba mbalimbali nchini zimekuwa zikiathiriwa na shughuli za binadamu kama vile kilimo na nyinginezo na kuhatarisha uwepo wa maeneo hayo na maisha ya wanyama kwa ujumla.
“Kumekuwa na changamoto katika uhifadhi wa shoroba na kama tunavyoona kuwa kuna zingine kuna makazi ya watu, shughuli za kilimo na kitu cha kwanza ambacho tunakiona ni kwamba kuna baadhi hazikuwa zimeainishwa.
“Zilikuwa hazijulikani kwa wananchi, kwahiyo watu wamekwenda wameweka makazi, shughuli za kilimo kwa sababu zilikuwa hazitambuliki,” alibainisha Mtaalamu huyo.
Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET), John Chikomo ameongeza kuwa katika mapambano dhidi ya changamoto za mabadiliko ya tabia nchi elimu ya mazingira na haswa uhifadhi bado inahitaji iepelekwe kwenye jamii.


