SINALOA, Mexico
HISTORIA ya Mexico na dawa za kulevya inaweza kuwa ilianzia mbali lakini wengi wanataja kipindi cha Vita vya Pili vya Dunia mwaka 1945 kama chanzo kikuu.
Kipindi hicho, viwanda vya Marekani vilikabiliwa na uhaba wa bangi na mimea mingine inayotumika kama kiungo cha uzalishaji wa dawa za matibabu ya binadamu.
Hivyo, katika kukabili uhaba huo, Marekani ikishirikana na Mexico ziliingia makubaliano. Kwamba zianzishe mashamba ya bangi huko Kaskazini-Magharibi mwa Mexico, hasa maeneo ya vijijini.
Wakulima katika maeneo ya milimani walilima na kuchakata bangi, kisha kusafirishwa kwenda Marekani kwa ajili ya kutengeneza dawa za kutibu wanajeshi waliokuwa vitani [Vita ya Pili ya Dunia].
Licha ya programu hiyo kumalizika baada ya Vita mwaka 1945, bado wakazi wa maeneo hayo walibaki na ujuzi wa kulima na kuchakata bangi, pia wakiwa tayari wana mitandao ya kuuza.
Kuanzia mwishoni mwa miaka ya 1960s hadi mwanzoni mwa miaka ya 1970, baadhi ya wazawa wakawa na uwezo wa kuuza na kusafirisha kiwango kikubwa zaidi cha bangi ndani na nje ya Mexico.
Wanahistoria na wataalamu wa masuala ya uhalifu wanaeleza kuwa huo ukawa mwanzo wa magenge ya biashara ya bangi, hasa katika Mji wa Sinaloa.
Baadaye, serikali ya Mexico ilikuja na opereshani mbalimbali, ikiwamo ya kuajiri wanajeshi na polisi zaidi 10,000 wa kuingia mitaani, kuwasaka na kuwakamata wauzaji wa bangi.
Hata hivyo, licha ya jitihada zote hizo, tayari mtandao wa uuzaji na usafirishaji wa bangi, sambamba na cocaine na heroine, ulishakuwa mkubwa na usioweza kudhibitiwa.
Wakati huo, Marekani nayo ilikuwa na operesheni za kutomokomeza magenge ya dawa hizo yaliyokuwa yameweka kambi katika Jimbo la Florida.
Hapo ndipo magenge hayo ya Colombia yalipoanza kuiona Mexico kama njia nzuri na rahisi zaidi kuingiza ‘mzigo’ nchini Marekani.
Mwanzoni mwa miaka ya 1980, makundi mawili makubwa nchini Colombia, Medellin Cartel na Cali Cartel, yalisimamia uzalishaji wa dawa, kisha kuyapatia magenge ya Mexico yaliyobeba na kuingiza Marekani.
Ni kipindi ambacho Miguel Angel Felix Gallardo aliyekuwa akiliongoza genge jingine kubwa la Guadalajara Cartel alikuwa akitajwa kuwa ndiye anayeratibu ‘mchongo’ mzima.
Utitiri wa magenge ya uhalifu ulionekana wazi baada ya Felix Gallardo kukamatwa na vyombo vya dola mwaka 1989.
Itaendelea …


