Na mwandishi wetu, Gazetini – ZANZIBAR
BAO la dakika ya 90 la Soufiane Bayazid limeipa MC Alger ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wenyeji wao, Yanga, katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliochezwa jioni ya leo Novemba 28, 2026, kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Bayazid amekuwa na kawaida ya kufunga mabao muhimu kwa MC Alger, kama alivyofanya msimu wa 2024-25 alivyopachika mabao matatu, likiwamo moja dhidi ya Yanga.
Safari hii, huo ulikuwa mchezo wa kwanza kwa kila timu kwenye Kundi B msimu huu wa michuano hiyo ya Shirikisho la Soka barani Afrika [CAF].
Katika mchezo huo, Yanga walionesha kiwango kizuri, licha ya kushindwa kuzitumia nafasi nyingi za wazi walizotengeneza.
Kwa kupoteza mchezo huo, Yanga wamepoteza rekodi yao nzuri ya mechi za nyumbani kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika.
Kabla ya kufungwa leo, vijana hao wa Kariakoo walikuwa wamepoteza mara moja tu katika mechi 21 walizocheza nyumbani tangu mwaka 2021.
Mara ya mwisho kwa mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara kufungwa mbele ya mashabiki wao kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ilikuwa mwaka 2024.


