Na mwandishi wetu, Gazetini-DAR
WAZIRI wa Nishati, Dk. Juma Homera, amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) katika kuimarisha upatikanaji wa umeme nchini, hatua inayochochea ukuaji wa viwanda, uwekezaji na uboreshaji wa huduma za kijamii.
Amesema Tanesco, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, imejipanga kuongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme kutoka vyanzo mbalimbali hadi kufikia megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030 ili kukidhi mahitaji yanayoendelea kuongezeka nchini.
Dk. Homera ameyasema hayo leo, Novemba 26, 2026, wakati wa maadhimisho ya miaka 95 ya Tanesco, akieleza kuwa safari ya shirika hilo imekuwa na historia ya maono, changamoto, mafanikio na ubunifu katika kuchangia maendeleo ya uchumi wa Tanzania kupitia nishati ya umeme.
Amesema katika kipindi ambacho Taifa linaendelea kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050, Tanesco ina nafasi muhimu katika kufanikisha mageuzi ya kiuchumi kupitia uwekezaji katika sekta ya nishati.
Waziri huyo ameipongeza Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti na wafanyakazi wa Tanesco kwa uzalendo, kujituma na mchango wao katika kuhakikisha huduma ya umeme inaendelea kuimarika na kuwafikia wananchi.
“Naipongeza Bodi na Menejimenti ya Tanesco kwa kazi kubwa ya kuhakikisha umeme unawafikia Watanzania. Tanesco ina mpango wa kuongeza uwezo wa uzalishaji umeme hadi kufikia megawati 8,000 mwaka 2030. Hatua hii inalenga kukidhi mahitaji ya umeme yanayoendelea kuongezeka na kuifanya Tanesco iendelee kuwa chombo muhimu katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii,” amesema Dk. Homera.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kutumia mifumo ya kisasa ya teknolojia katika utoaji wa huduma za umeme ili kurahisisha upatikanaji wake kwa wananchi wengi zaidi na kuongeza ufanisi wa shughuli za shirika hilo.
Tanesco ilianzishwa Novemba 26, 1931, na leo inaadhimisha miaka 95 tangu kuanzishwa kwake, ikiwa imepiga hatua katika shughuli za uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme nchini.


