14.8 C
New York

Koffi Olomide: Historia na Tanzania, kolabo zake Bongo Fleva – [8]

Published:

KINSHASA, DRC

HISTORIA inakumbusha kuwa Koffi amekuwa na uhusiano wa karibu na Tanzania, tena uliodumu kwa miaka mingi, akiingia nchini kwa mara ya kwanza mwaka 1993.

Wakati huo, aliingia Tanzania kutangaza albamu yake ya ‘Noblesse Oblige’ iliyokuwa na nyimbo nyingi kali, ikiwamo ‘Papa Plus’. Tangu hapo, amekuwa akiingia na kutoka Tanzania.

Hata hivyo, kwa mara ya kwanza, alitia mkono kwenye kiwanda cha muziki wa kizazi kipya nchini [Bongo Fleva] mwaka 2020 baada ya kufanya kolabo ya maana na staa Abdul Nasseb ‘Diamond Platnumz’.

Itakumbukwa, Diamond, bosi wa lebo ya muziki ya WCB, alimshirikisha mkongwe huyo katika wimbo ‘Waah’, ambao ulifanya vizuri ndani na nje ya Tanzania na Ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.

Mwaka uliofuata, Februari 11, 2021, Koffi aliingiza tena sauti yake ya gharama kwenye muziki wa Bongo Fleva, safari hii akipewa kolabo na Nandy ‘African Princess’ katika ngoma iitwayo ‘Leo Leo’.

Miaka miwili baadaye, Koffi akarudi Bongo Fleva na kukutana na Diamond. Safari hii, wakaachia kigongo kingine kiitwacho ‘Achii’ kilichotoka Agosti 15, 2023.

Kwa ufupi, Koffi amefanya kolabo tatu na wasanii wa Bongo Fleva, huku kumbukumbu zikionesha kuwa ameingia Tanzania mara zaidi ya 20, hivyo kuwa moja ya nchi alizotembelea zaidi.

Historia inamtambua Koffi kwa nyimbo zake nyingi zilizowahi kufanya vizuri barani Afrika, lakini haitoacha kuzigusa ‘Loi’, ‘Fouta Djallon’, ‘Heros National’, ‘Effrakata’ na ‘Ekoti te’, maarufu zaidi kwa jina la ‘Selfie’.

Vilevile, Koffi si tu mmoja ya wanamuziki wa Afrika waliouza nakala nyingi, achilia mbali kuwa msanii pekee aliyeweza kubeba tuzo nne za Kora kwa mpigo, pia kuna rekodi nyingine kali anayoishikilia.

Ndiyo, Koffi ndiye msanii pekee kutoka katika ardhi ya DRC ambaye albamu yake ipo kwenye Kitabu cha ‘1001 Albums You Must Hear Before You Die’ [Albamu 1001 Unazopaswa Kusikiliza Kabla Hujafa].

Mwisho …

Related articles

Recent articles