14.2 C
New York

Tanesco yabuni njia mpya ya kurejesha umeme Mbagala, Pwani

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

WATAALAMU wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) wamefanikiwa kujenga kwa haraka njia mpya ya muda ya kusafirisha umeme kwa kutumia miundombinu ya juu ya ardhi (overhead), hatua inayolenga kupunguza athari za hitilafu ya njia ya chini ya ardhi ya msongo wa kilovoti 132 (132kV) iliyojitokeza Gongolamboto na kuathiri upatikanaji wa umeme katika maeneo ya Mbagala, Kigamboni, Mkuranga na Kibiti.

Ujenzi wa njia hiyo mbadala unatajwa kuwa suluhisho la dharura lililobuniwa na wataalamu wa Tanesco ili kuruhusu umeme kuendelea kusafirishwa huku ukivuka eneo lenye miundombinu ya Reli ya Kisasa (SGR), wakati matengenezo ya njia ya chini ya ardhi iliyopata hitilafu yakiendelea.

Hatua hiyo inakuja baada ya changamoto ya kiufundi iliyojitokeza Novemba 3, 2026, katika njia inayounganisha Kituo cha Kupokea na Kupoza Umeme cha Gongolamboto na vituo vya Mbagala na Dege, Kigamboni, na kuathiri huduma ya umeme katika maeneo yaliyokuwa yakitegemea njia hiyo.

Akizungumza Novemba 7, 2026, wakati akikagua maendeleo ya matengenezo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Lazaro Twange (pichani), amewapongeza wataalamu wa Shirika hilo kwa kubuni na kutekeleza kwa haraka suluhisho hilo la muda, akisema hatua hiyo inalenga kuhakikisha wateja wanaendelea kupata huduma ya umeme wakati miundombinu iliyoharibika ikirekebishwa.

“Tumefika hapa kukagua maendeleo ya kazi na kujionea hatua zinazochukuliwa na wataalamu wetu. Tumefarijika kuona kuwa wameweza kutengeneza njia nyingine mbadala ya juu inayovuka eneo la SGR ili kuhakikisha umeme unaendelea kusafirishwa na kuwafikia wateja wetu wakati matengenezo ya njia ya ardhini yakiendelea. Tunawahakikishia wateja wetu kuwa tunaendelea kufanya kila linalowezekana kuhakikisha wanapata huduma ya umeme,” amesema Twange.

Awali, maeneo yaliyoathirika yalikuwa yakitegemea pia njia nyingine mbadala iliyokuwepo, lakini uwezo wake mdogo wa kubeba mahitaji yote ya umeme kwa wakati mmoja ulifanya baadhi ya wateja kuendelea kukabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa huduma hiyo.

Kwa mujibu wa Tanesco, wataalamu wanaendelea na kazi za kuunganisha na kukamilisha mfumo huo mpya wa muda, huku wakizingatia taratibu za kiufundi na usalama kabla ya kuanza kutumika kikamilifu.

Twange amesema Shirika linaendelea kuchukua hatua za kuimarisha miundombinu ya umeme na kutafuta suluhisho za kupunguza athari kwa wateja kila changamoto ya kiufundi inapojitokeza.

Tanesco inaendelea na matengenezo ya njia ya chini ya ardhi ya 132kV kwa lengo la kurejesha mfumo wake katika hali ya kawaida na kuimarisha uhakika wa upatikanaji wa umeme katika maeneo yanayotegemea miundombinu hiyo.

Related articles

Recent articles