MADRID, Hispania
HISPANIA itajiondoa kuandaa michuano ya Kombe la Dunia ya mwaka 2030 endapo haitopewa nafasi ya kuwa mwenyeji wa mchezo wa fainali.
Ifahamike kuwa Hispania ni mwenyeji mwenza wa mashindano hayo kwa kushirikiana na Morocco na Ureno.
Kwa mujibu wa mmoja ya wagombea wa nafasi ya Waziri Mkuu katika Uchaguzi Mkuu ujao wa Hispania, atahakikisha nchi hiyo inajitoa ikiwa Morocco ndiyo itakayopewa heshima ya kuandaa mechi ya mwisho.
Mgombea huyo wa Chama cha Partido Popular, Alberto Nunez Feijoo, amesisitiza kuwa mechi ya fainali inapaswa kuchezwa nchini Hispania na si vinginevyo.
Kwa sasa, Uwanja wa Hassan II ulioko mjini Casablanca na wenye uwezo wa kupokea mashabiki 115,000 ndiyo unaopewa nafasi kubwa ya kutumika siku ya fainali.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Nunez Feijoo, fainali inapaswa kuchezwa katika Uwanja wa Santiago Bernabeu au Camp Nou.


