Na mwandishi wetu, Gazetini
MANISPAA ya Kahama mkoani Shinyanga imetoa mikopo isiyo na riba yenye thamani ya Shilingi bilioni 2.1 kwa vikundi 96 vya wanawake, vijana na wenye ulemavu.
Katika mikopo hiyo, vikundi vya wanawake 46 vimepokea Shilingi milioni 708, vikundi vya vijana 45 vimepokea Shilingi bilioni 1.42, huku wenye ulemavu watano wakipewa Shilingi milioni 31.
Mikopo hiyo imetolewa leo Novemba 5, 2026 kupitia mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Manispaa ya Kahama katika Robo ya Kwanza na ya Pili ya Mwaka wa Fedha 2026-2027.
Akikabidhi mfano wa hundi, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, amevitaka vikundi vilivyopata mikopo hiyo kuitumia kujijenga kiuchumi ili kuondokana na utegemezi katika jamii.
Aidha, Mhita amewaonya vijana kuepuka kuhonga fedha za mkopo wanazopewa na badala yake ziendane na malengo waliyojiwekea.
“Lengo la Serikali ni kuweka mazingira wezeshi kwa wananchi wake kushiriki shughuli za uzalishaji mali, kujiajiri na kuongeza kipato. Utoaji wa mikopo isiyo na riba kwa makundi haya ni programu yenye mchango muhimu kwa Taifa letu katika kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050,” amesema.
Wakati huo huo, Mkuu Mkoa huyo amezielekeza Halmashauri kutoa kipaumbele kwa vikundi vyenye uwezo wa kufanya shughuli zinazotangazwa ili kuvikuza na kuvifanya viaminike zaidi.
Katika hatua nyingine, Meya wa Manispaa ya Kahama, Mataluma Kaniki, amesema Baraza la Madiwani kwa kushirikiana na wataalamu wa Halmashauri limejipanga kuhakikisha ifikapo Juni, 2027, inatoa mikopo isiyopungua Shilingi bilioni 4 kwa makundi hayo maalumu.
Mmoja wa wanufaika wa mikopo hiyo, Adam Mohamed, ameishukuru Serikali kwa hatua hiyo akisema itamsaidia kujikwamua kiuchumi na kuondokana na fedheha aliyokuwa akikutana nayo kutokana na umasikini.
“… Mimi mwenye ulemavu ilikuwa nikimsalimia tu mtu ananiona nataka kumuomba, lakini leo Serikali imeona umuhimu wa kutukopesha mlemavu mmoja mmoja, tumeonwa na tunafarijika sana,” amesema.


