13.9 C
New York

NIDA yatajwa kukwamisha mbegu za pamba

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini-Kishapu

MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Josephat Limbe, ameiagiza Bodi ya Pamba kutafuta suluhisho la changamoto ya usajili wa namba za Utambulisho wa Taifa (NIDA) kwa wakulima, huku akisisitiza kuwa ukosefu wa namba hizo usiwe kikwazo kwa wakulima kupata mbegu za pamba.

Akizungumza Oktoba leo Alhamisi, 29, 2026, wakati wa Baraza la Madiwani lililojadili utekelezaji wa shughuli za maendeleo kwa robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/2027, lililofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Limbe pia amewataka viongozi wa NIDA kusogeza huduma za usajili karibu na wananchi wa vijijini ili kuhakikisha wote wanapata namba za utambulisho.

“Namba za NIDA zisiwe kigezo cha wakulima kukosa mbegu za pamba. Bodi ya Pamba, tafuteni suluhisho mapema kuhakikisha wakulima wote wanapata mbegu kwa wakati. Bila hivyo, tunadhoofisha zao la pamba,” amesema Limbe.

Ameongeza kuwa NIDA inapaswa kuhakikisha huduma za usajili zinawafikia wananchi katika kata zote, akieleza kuwa namba hizo ni muhimu si kwa upatikanaji wa pembejeo za kilimo pekee, bali pia kwa utambulisho wa wananchi.

“Watu wa NIDA, hakikisheni mnafika katika kata zote ili wananchi wajiandikishe na kupata namba. NIDA haitumiki kwenye pembejeo tu, bali ni utambulisho wa Mtanzania,” amesema Limbe.

Akijibu maelekezo hayo, Mkaguzi wa Bodi ya Pamba Tanzania katika Wilaya ya Kishapu, Joachim Gobanya, amesema amepokea agizo la kutafuta njia mbadala ya kuwawezesha wakulima kupata mbegu za pamba bila kutegemea namba za NIDA.

“Nimepokea maagizo ya kutafuta hatua nyingine itakayoweza kutumika kuwapa wakulima mbegu. Hata hivyo, bado tuko ndani ya muda wa kutoa mbegu kwa wananchi. Hii pia inasaidia kupunguza uwezekano wa wakulima kutumia mbegu hizo kwa shughuli nyingine, kama vile kulishia mifugo, endapo zingetolewa mapema,” amesema Gobanya.

Changamoto hiyo imeibuliwa kupitia taarifa za makatibu wa madiwani wa CCM na ACT-Wazalendo, zilizowasilisha hoja na kero za wananchi. Miongoni mwa changamoto zilizoelezwa ni kuchelewa kupatikana kwa mbegu za pamba na ugumu wa wakulima kupata namba za NIDA.

Akiwasilisha hoja hiyo, Katibu wa ACT-Wazalendo ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Bunambiyu, Adrian Ngele, amesema wakulima wanahitaji huduma za usajili wa NIDA zisogezwe karibu na maeneo yao ili kupunguza gharama za kufuata huduma hizo katika halmashauri.

“Wakulima wanauliza ni lini watasogezewa huduma za usajili wa NIDA katika kata zetu. Ufuatiliaji wake kwa kwenda halmashauri ni mgumu kutokana na umbali, na hali hii inasababisha wakulima kukosa vigezo vya kupata pembejeo za kilimo, hasa mbegu,” amesema Ngele.

Kwa upande wake, Katibu wa Madiwani wa CCM ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Songwa, Abdul Ngoromole, amesema wakulima wamekuwa wakikosa mbegu za pamba kutokana na kutokidhi vigezo vinavyohitajika, huku ukosefu wa namba za NIDA ukiwa miongoni mwa vikwazo vikuu.

“Tumekuwa na changamoto ya kukosa mbegu za pamba kwa sababu hatujakidhi vigezo, na kizuizi kikubwa ni namba za NIDA ambazo wakulima wengi hawana. Hamuoni kuwa hali hii inaweza kushusha uzalishaji na kudhoofisha zao la pamba?” amehoji Ngoromole.

Naye Diwani wa Kata ya Seke Bogoro, Frednand Mpogomi, amesema wakulima katika kata yake pia wanalalamikia gharama za kufuata huduma za NIDA katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu.

Amesema mkulima mmoja anaweza kutumia takribani Shilingi 20,000 kwa safari ya kwenda na kurudi halmashauri, umbali unaozidi kilomita 70, hali inayowawia vigumu wananchi wengi wa vijijini kumudu gharama hizo.

Kutokana na changamoto hizo, viongozi hao wamehimiza hatua za kusogeza huduma za NIDA karibu na wananchi na kutafuta suluhisho litakalowezesha wakulima kupata mbegu za pamba kwa wakati, ili kulinda uzalishaji na kuimarisha zao hilo muhimu kiuchumi.

Related articles

Recent articles