12.9 C
New York

Tanzania, Angola kuanzisha safari za anga za moja kwa moja

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania na Angola zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta ya usafiri na usafirishaji, ikiwemo kuanzisha safari za moja kwa moja za anga kati ya nchi hizo mbili kwa lengo la kukuza biashara, uwekezaji na utalii.

Akizungumza Ikulu jijini Dar es Salaam, leo, Alhamisi, Oktoba 29, 2026, baada ya mazungumzo na Rais wa Angola, João Manuel Gonçalves Lourenço, Rais Samia amesema nchi hizo zimetia saini mkataba wa huduma za usafiri wa anga utakaowezesha kuanzishwa kwa safari hizo.

Amesema changamoto za usafiri zimekuwa miongoni mwa vikwazo vinavyoathiri ukuaji wa biashara baina ya Tanzania na Angola, hivyo wamekubaliana kuimarisha ushirikiano katika usafiri wa anga, reli na majini.

Aidha, amesema nchi hizo zinaendelea kuweka mazingira ya kuunganisha shoroba za usafirishaji za Lobito na Dar es Salaam, hatua inayotarajiwa kuungwa mkono na kukamilika kwa miradi ya ukarabati wa reli ya TAZARA na reli ya Benguela nchini Angola.

Kwa mujibu wa Rais Samia, kukamilika kwa miradi hiyo kutarahisisha usafirishaji wa bidhaa na kuimarisha muunganiko wa kiuchumi kati ya nchi hizo pamoja na maeneo jirani.

Vilevile, amesema Tanzania na Angola zimekubaliana kuandaa kongamano la biashara na uwekezaji litakalowakutanisha wafanyabiashara na wadau wa sekta binafsi kutoka nchi hizo mbili, kwa lengo la kubaini fursa mpya za ushirikiano na kuongeza biashara.

Rais Samia amesisitiza kuwa hatua hizo zinalenga kuimarisha uhusiano wa kihistoria kati ya Tanzania na Angola na kuugeuza kuwa fursa za maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wa nchi hizo mbili.

Related articles

Recent articles