14 C
New York

Christophe Gleizes; Mfungwa aliyeibukia Ballon d’Or

Published:

LONDON, Uingereza

CHRISTOPHE Gleizes mwenye umri wa miaka 37, ni mwandishi wa habari raia wa Ufaransa, ambaye amejikita katika uandishi na uchambuzi wa soka la Afrika katika jarida la michezo la So Foot la jijini Paris.

Kwa sasa, mwandishi huyo anasota gerezani akitumikia kifungo cha miaka saba nchini Algeria.

Sasa, wakati wa hafla ya utoaji wa tuzo ya Ballon d’Or yam waka huu iliyofanyika jijini London mapema wiki hii, jina lake lilichomoza.

Katika televisheni kubwa iliyokuwa ukumbini wakati wa hafla ya Ballon d’Or, ulionekana ujumbe ukieleza kuwa Gleizes amekuwa jela kwa mwaka mmoja, miezi mitatu na siku 27.

“Ballon d’Or na familia ya soka ya Ufaransa ingependa kutumia nafasi hii kuifanya sherehe hii kuwa maalumu kwa Christophe Gleizes,” alisema mtangazaji wa Uingereza, Kate Scott, aliyekuwa mshereheshaji [MC] akishirikiana na lejendari wa Ufaransa, Thierry Henry.

Gleizes alikamatwa na mamlaka za Algeria mwaka 2024 alipotembelea nchini humo kuripoti juu ya klabu maarufu ya soka ya Jeunesse Sportive de Kabylie (JSK). Mamlaka za nchi hiyo zilieleza kuwa mwandishi huyo anajihusisha na ugaidi.

Klabu hiyo iko Tizi Ouzou, umbali wa kilometa 100 kutoka Mji Mkuu wa Algiers. Wenyeji wa eneo hilo ni wa jamii ya Amazigh, zamani wakifahamika kwa jina la ‘Berbers’.

Pia, ni eneo ambalo ndiko yaliyo makao makuu ya Movement for the Self-Determination of Kabylie (MAK), kundi ambalo mamlaka za Algeria zilitangaza kulihusisha na ugaidi mwaka 2021.

Baada ya kutiwa nguvuni, ilielezwa kuwa Gleizes alikuwa akichakata nyaraka zilizolenga kujenga chuki kati ya serikali ya Algeria na wananchi wake, hivyo kutikisa usalama wa taifa.

Wakati huo, Gleizes alitajwa kuwa na ukaribu na mmoja ya viongozi wa klabu ya JSK, ambaye pia alishashukiwa mara kadhaa na vyombo vya dola kuwa ana ukaribu na Kundi la MAK.

Waendesha mashitaka walikazia kuwa hata safari yake nchini Algeria haikuwa kwa ajili ya kutelekeza majukumu ya uandishi wa habari, bali alikwenda kwa mpango maalumu kwa kushirikiana na magaidi hao.

Kwa upande mwingine, Gleizes ni mfano tu wa waandishi wa habari waliowahi kuingia matatani na hata kufungwa jela nchini Algeria wakihusishwa na vitendo vya kigaidi.

Ikumbukwe, mwandishi raia wa Algeria mwenye asili ya Ufaransa, Boualem Sansal, alihukumiwa kifungo cha miaka mitano gerezani, kabla ya kuponea msamaha wa Rais Abdelmadjid Tebboune baada ya mazungumzo yake na Rais wa Ujerumani mwaka 2025.

Wakati Gleizes anakamatwa, tayari ulikuwepo uadui kati ya Ufaransa na Algeria, ingawa uhusiano wao umeonekana kuimarika katika siku za hivi karibuni.

Mei, 2026, Waziri wa Sheria wa Ufaransa, Gerald Darmanin, alifanya ziara yake ya kikazi mjini Algiers na kuitaka Algeria kumwachia huru Gleizes, ombi ambalo hata hivyo halijapokelewa hadi sasa.

Related articles

Recent articles