Na Hassan Mwasha, Gazetini
OKTOBA 14 ya kila mwaka ni siku maalumu ya kumbukizi ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyefariki akiwa kwenye matibabu ya saratani katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas jijini London.
Kwa upande mwingine, Oktoba 14 imebaki kuwa nembo muhimu ya mchango mkubwa aliokuwa nao Mwalimu Nyerere katika nyanja za kisiasa, kiuchumi na kijamii kwa ujumla wake.
Kama ilivyo kawaida, Watanzania huitumia siku hiyo kujikumbusha, kukumbushana na kuitangazia dunia namna Mwalimu Nyerere alivyotumia sehemu kubwa ya uhai wake kupigania maendeleo ya nyanja hizo.
Aidha, Oktoba 14 pia imekuwa ni siku muhimu ya kujitafakari kama Taifa, kuona hatua zilizopigwa katika kuyalinda na kuyaenzi maono ya Rais huyo wa kwanza.
Je, ikiwa ni miaka 27 imepita tangu Mwalimu alipoiacha dunia, ni yapi yangemshangaza endapo angerudi leo hii? Makala haya yanachambua.
Udini
Hakuna ubishi kuwa Mwalimu hakuwa muumini wa jamii iliyogawanyika kwa misingi ya dini, kabila, rangi ya ngozi, au hali ya kiuchumi. Alisisitiza umoja na mshikamano, bila kujali tofauti hizo na alifanikiwa.
Kwa miaka ya hivi karibuni, ni kama Tanzania imeanza kuachana na misingi hiyo. Mara kadhaa imeshuhudiwa minyukano ya wazi kati ya waumini wa dini kubwa mbili; Uislam na Ukiristo.
Kwa upande wake, mchambuzi wa siasa nchini, Dkt. Richard Mbunda, anaamini mzizi wa tatizo ni taasisi za dini kutumika kwa masilahi ya kisiasa.
“Chanzo siyo dini, bali ni masilahi ya kisiasa. Ni mbaya na ingemuumiza Mwalimu kuona dini zinavyotumika katika siasa. Watu wa dini fulani wanamkingia kifua kiongozi kwa sababu tu anatoka kwenye dini yao.
“Akikosolewa, wanamtetea pasi na kupima hoja. Kiongozi naye akikosolewa na watu wa dini yake, atakaa kimya, lakini akiguswa na wa dini nyingine anakuwa mkali.
“Huwezi kujenga nchi ya amani katika mazingira ya aina hii. Leo ni miaka 26 tangu tulipoingia karne ya 21, ni aibu kuona mipasuko ya udini.”
Maadili utumishi wa umma
Hili ni eneo jingine alilosisitiza Mwalimu katika hotuba zake nyingi, akiwataka viongozi wa umma kutumia nafasi zao kwa masilahi mapana ya watu na nchi yao. Mwalimu aliamini kiongozi ni ‘mtumwa’ kwa watu anaowaongoza.
Kinyume chake, miaka ya hivi karibuni imeshuhudia anguko la maadili kwa watumishi wa umma, hilo likithibitishwa na ‘upigaji’ unaoibuliwa kila inapotoka Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali [CAG].
“Mwalimu angeshangaa. Maadili ya utumishi wa umma yangemshtua kwa kweli. Kwa sasa viongozi hawalindi tena masilahi ya nchi, bali wanajinufaisha wao, familia zao na watu wao wa karibu,” anasema Dkt. Mbunda.
Siasa za upinzani
Miaka 27 tangu Mwalimu alipofariki, siasa za upinzani nchini zina sura tofauti na ile aliyoiacha mwaka 1999. Kwa sasa, si CUF tena, bali CHADEMA ndicho Chama cha upinzani chenye nguvu zaidi. Chama alichokiacha kikiwa bado kichanga.
“Mwalimu ni miongoni mwa viongozi wachache waliopeda siasa za upinzani, licha ya ukweli kwamba wengi ndani ya CCM [Chama cha Mapinduzi] walikataa,” Dkt. Mbunda anasema.
“Aliamini ili CCM iweze kujisahihisha, lazima kuwe na upinzani mzuri. Kama Mwalimu angekuwa hai leo hii, basi angeipongeza CHADEMA na hata kusikitika kwa changamoto kinazopitia.”


