17.6 C
New York

Kweka anayedaiwa kumuua mkewe kortin

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

MFANYABIASHARA na mkazi wa Bunju A, Laurence Kweka (48), amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, akikabiliwa na shtaka moja la mauaji ya mkewe, Jane Maloo Urassa, kwa kumpiga risasi.

Kweka amesomewa shtaka hilo leo, Alhamisi, Oktoba 15, 2026, na Wakili wa Serikali, Harrison Lukosi, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Kemilembe Josiah.

Akisoma shtaka hilo katika kesi ya mauaji namba 23407 ya mwaka 2026, Lukosi alidai kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Oktoba 1, 2026, katika eneo la Bunju A, Wilaya ya Kinondoni, mkoani Dar es Salaam, kwa kumuua Jane Maloo Urassa.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, kosa hilo linadaiwa kukiuka vifungu vya 196 na 197 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, iliyofanyiwa marejeo mwaka 2023.

Kabla ya kusomewa shtaka hilo, Hakimu Josiah alimweleza mshtakiwa kuwa hatakiwi kujibu shtaka hilo katika mahakama hiyo kwa kuwa haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji.

Aidha, mahakama ilieleza kuwa shtaka la mauaji halina dhamana kwa mujibu wa sheria, hivyo mshtakiwa ataendelea kubaki rumande wakati upelelezi ukiendelea.

Wakili Lukosi aliiomba mahakama kupanga tarehe nyingine ya kutajwa kwa kesi hiyo, akieleza kuwa upelelezi bado haujakamilika.

Hakimu Josiah aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 29, 2026, kwa ajili ya kutajwa, huku mshtakiwa akiendelea kubaki rumande.

Related articles

Recent articles