15.1 C
New York

Vigogo EPL presha inapanda, inashuka

Published:

LONDON, Uingereza

ARSENAL walifungua pazia la msimu huu wa Ligi Kuu ya England [EPL] wakiwa na matajirio ya kutetea ubingwa wao. Manchester City, Liverpool na Chelsea walianza wakiwa na makocha wapya kwenye mabenchi yao ya ufundi.

Kwa upande wao, baada ya kumaliza katika nafasi ya tatu msimu uliopita, Manchester United walitamani kuanzia pale walipoishia. Tottenham walitamani ‘kufufuka’ baada ya kunusurika kushuka Daraja msimu uliopita [2025-26].

Tottenham

Kwa misimu miwili mfululizo, Tottenham wameishia nafasi ya 17 kwenye msimamo wa EPL. Baada ya kutumia zaidi ya Pauni milioni 300 kwenye usajili wa kiangazi, timu hiyo ilitarajiwa kuanza vizuri msimu huu wa 2026-27.

Tofauti na matarajio hayo, Tottenham wako mkiani mwa msimamo baada ya kukusaya pointi mbili tu katika mechi tano walizocheza.

Mbaya zaidi, timu hiyo imefunga mabao mawili pekee, tena katika mchezo uliopita wa kichapo cha mabao 3-2 kutoka kwa Aston Villa.

Manchester United

Baada ya kushika nafasi ya tatu msimu uliopita, safari hii matarajio yalikuwa makubwa kwa kocha Michael Carrick. Walianza msimu kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Hull City.

Tangu hapo, mambo yamekuwa mabaya kwa ‘Mashetani Wekundu’ kwani hiyo ndiyo mechi pekee waliyoshinda, wakipoteza mbili, sare mbili na kukusanya pointi tano pekee.

Mwenendo mbovu wa timu hiyo kwenye Ligi umemuweka kwenye hali mbaya Carrick na zipo tetesi kuwa atafukuzwa endapo mambo hayatokaa sawa katika mechi zijazo.

Chelsea

Chini ya kocha mpya, Xabi Alonso, mambo hayajawa mazuri kwa Chelsea msimu huu. Waliuanza vizuri msimu huu kwa ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Fulham [Agosti 24, 2026].

Kabla ya mapumziko ya kalenda ya FIFA [Shirikisho la Soka la Kimataifa], Chelsea haikuwa imepata ushindi katika mechi tatu mfululizo kwenye Ligi, na badala yake ilifungwa mbili na sare moja.

Blues wako nafasi ya 10 kwenye msimamo, wakiwa wameruhusu nyavu zao kutikiswa mara 12. Kwa ufupi, ndiyo timu iliyofungwa mabao mengi zaidi msimu huu wa EPL.

Liverpool

‘Majogoo’ wa Anfield wako chini ya kocha mpya, Andoni Iraola, ambaye aliajiriwa kuchukua nafasi ya Arne Slot, ambaye msimu uliopita alipoteza mechi 20 kwenye Ligi.

Chini ya Iraola, Liverpool haijaonja kichapo msimu huu lakini wako nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi baada ya kukusanya pointi tisa katika mechi zao tano.

Aidha, kocha huyo wa zamani wa Bournemouth amefanikiwa ‘kufufua’ makali ya straika Alexander Isak, ambaye ameshafunga mabao manne ya Ligi msimu huu.

Arsenal

Mabingwa watetezi hao wa taji la EPL wameshakusanya pointi 12 katika mechi tano. Wameshinda nne na kufungwa moja, hivyo bado wana matumaini ya kuendeleza moto wao wa msimu uliopita.

Hata hivyo, bado kocha Mikel Arteta ana kazi kubwa ya kufanya kwani vijana wake wamekuwa na kiwango kisichoridhisha katika baadhi ya mechi, licha ya kupata ushindi.

Katika mechi yao ya mwisho kabla ya mapumziko ya FIFA, walitandikwa mabao 3-0 na Brighton, matokeo yaliyoibua maswali juu ya ubora wa kikosi hicho.

Manchester City

Baada ya kuachana na Pep Guardiola mwishoni mwa msimu uliopita [2025-26], Man City kwa sasa iko chini ya kocha mpya aliyewahi kuinoa Chelsea, Enzo Maresca.

Licha ya kiungo wake tegemeo na mshindi wa Ballon d’Or, Rodri, kutimkia Barcelona, Man City imeshinda mechi zote tano za msimu huu wa EPL na kwa sasa iko kileleni mwa msimamo.

Tangu ilipofungwa mabao 3-0 na Arsenal kwenye Ngao ya Jamii, Man City imeshinda mechi zote saba za mashindano yote inayoshiriki.

Related articles

Recent articles

VAR bado kizungumkuti EPL