MADRID, Hispania
KYLIAN Mbappe ameachana na kampuni ya vifaa vya michezo ya Nike baada ya kuwa balozi wake kwa miaka 20. Staa huyo wa Real Madrid amejiunga na kampuni ya On ya nchini Uswis.
Hilo ni pigo kubwa kwa Nike kwani Mbappe anakuwa staa mwingine kuikacha baada ya Lamine Yamal wa Barcelona kuondoka na kujiunga na Adidas mwaka 2024.
Mbappe alikuwa na ofa nono kutoka kwa wapinzani wakubwa wa Nike, Adidas na Puma, lakini ‘alizipotezea’ na kuichagua On ambayo hata hivyo si maarufu sana kwenye ulimwengu wa soka.
Hata hivyo, On ni kampuni ambayo Mkurugenzi wake wa Soka ni lejendari wa timu ya Taifa ya Ufaransa, Thierry Henry, na hiyo inaweza kuwa imemshawishi Mbappe kuichagua.
On ilianzishwa mwaka 2010 mjini Zurich, na matajiri watatu wa Uswis, Olivier Bernhard, David Allemann na Caspar Coppetti. Mwaka 2019, staa wa tenesi, Roger Federer, alinunua hisa na sasa ni mmoja ya wamiliki.
Mshambuliaji wa Barcelona na Uswis, Sydney Schertenleib, alikuwa mchezaji wa kwanza [wa sasa] kupewa ubalozi na kampuni hiyo Desemba, 2025.
Ripoti zinaeleza kuwa Mbappe alikuwa akivuna euro milioni 14 katika mkataba wake wa kutangaza bidhaa za Nike. Kwa miaka 20, alivaa aina 12 tofauti za viatu vya kampuni hiyo.
Miongoni mwa viatu hivyo ni Mercurial Superfly 11 vilivyonakshiwa kwa madini ya dhahabu, ambavyo alivitumia wakati wa Kombe la Dunia [2026] na kutwaa tuzo ya mfungaji bora akiwa na mabao 10 na ‘asisti’ nne.
Kwa upande wa mkataba wake na On, hakuna taarifa rasmi juu ya atavuna kiasi gani, ingawa zipo taarifa zinazodai kuwa huenda naye akawa amepewa hisa, kama ilivyo kwa Federer.


