Na mwandishi wetu, Gazetini
HISTORIA ya siasa za Afrika itaendelea kumkumbuka kama kielelezo cha viongozi wachache waliowahi kutumia vibaya nafasi zao.
Alikuwa rais wa Liberia kuanzia Agosti 2, 1977, hadi alipojiuzulu Agosti 11, 2003, kisha kuhukumiwa kifungo cha miaka 50 gerezani mwaka 2012.
Anaendelea kutumikia adhabu hiyo hadi sasa, chanzo kikiwa ni kuhusika kwake katika uhalifu dhidi ya binadamu wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe katika nchi jirani ya Sierra Leone [1991–2002].
Huyo ndiye Charles Taylor na makala haya yanakuletea mfululizo wa simulizi ya maisha yake binafsi, hatua zake kwenye ulingo wa siasa, na anguko lake. Karibu.
Historia inaanza hivi; Mwaka 1871, raia wa Marekani aitwaye Jefferson Bracewell aliongozana na familia yake ndogo kuhamia Arthington, Liberia, wakitokea nchini kwao, Marekani.
Akiwa Liberia, Bracewell na familia yake walijichanganya na wenyeji wao katika shughuli za kilimo cha kahawa, pamba, miwa, nyanya na mchele ili maisha yaendelee.
Miaka mingi baadaye, mjukuu wa Bracewell, Neilson alianzisha uhusiano wa kimapenzi na mfanyakazi wao wa ndani raia wa Liberia, Yassa Zoe Louise, na hapo ndipo inapoanzia historia ya Taylor.
Baada ya uhusiano wa muda, Neilson alimpachika mimba Yassa na kisha kufunga naye ndoa. Hata hivyo, kutokana na ubaguzi wa rangi, ikizingatiwa kuwa familia ya Neilson ilikuwa ya kizungu [Marekani], haikuvutiwa kuona mtoto wao akiwa na mwanamke mweusi.
Licha ya changamoto hiyo, Neilson na Yassa waliendelea na maisha yao mjini Arthington, jirani na Mji Mkuu wa Monrovia, na wakiwa na watoto watatu, familia yake iliamua kumchukua wa mwisho ambaye ndiye Taylor aliyezaliwa Januari 28, 1948.
Uamuzi wa familia ya Neilson kumchukua Taylor ulilenga kumsaidia malezi bora zaidi, ikiwamo kumpatia elimu nzuri na fursa nyingi za kimaisha. Miaka ilisogea na hatimaye Taylor alihitimu Shahada ya Uchumi katika Chuo Kikuu cha Bentley, Marekani, mwaka 1977.
Aliporejea Liberia, Taylor aliunga mkono mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na Samuel Doe mwaka 1980. Mapinduzi yaliyosababisha kuuawa kwa Rais William Tolbert. Doe akajitangaza kuwa rais wa nchi hiyo.
Katika serikali mpya, Doe alimteua Taylor kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Huduma la Taifa [GSA], nafasi ambayo alihusika kuratibu manunuzi yote ya Serikali.
Alidumu kwenye kiti kwa miaka mitatu pekee, kisha ‘akatumbuliwa’ na kufunguliwa mashitaka ya ubadhirifu, akitajwa ‘kupiga’ Dola milioni moja. Mashitaka hayo yalisababisha Taylor akimbilie Marekani lakini alikamatwa Mei 21, 1984.
Akiwa gerezani kusubiri hatima yake, Taylor alishirikiana na wafungwa wanne kutoroka mwaka 1985, ikielezwa kuwa walipata upenyo baada ya kuvunja nondo za dirisha, kisha kuruka uzio na kutokomea.
Wakati wa hukumu yake ya mwaka 2012, Taylor aliiambia mahakama kuwa alifanikiwa kutoroka baada ya kusaidiwa na baadhi ya majasusi wa Marekani [CIA]. Awali, Marekani iliwahi kukiri kumtumia katika masuala ya kijasusi, ingawa haikueleza ni kwa namna gani.
Taylor alipoondoka gerezani, aliibukia Libya iliyokuwa chini ya Muammar Gaddafi wakati huo. Vyanzo vinaeleza kuwa huko ndiko alikopatiwa mafunzo ya uasi wa vita vya msituni.
Baadaye, aliondoka Libya na kuweka kambi Ivory Coast na kuanzisha kundi la National Patriotic Front of Liberia [NPFL] akiwa hapo.
NPFL iliingia Liberia na kuanzisha mashambulizi dhidi ya Serikali ya Rais Doe, hatua hiyo ikisababisha Vita vya Kwanza vya Wenyewe kwa Wenyewe [First Liberian Civil War]. Kufikiam waka 1990, NPFL ilikuwa ikidhibiti maeneo mengi ya nchi.
Hata hivyo, mwaka huo huo, Taylor alipata pigo zito baada ya aliyekuwa Kamanda wake, Prince Johnson, kujitenga na kuanzisha kundi lake la Independent National Patriotic Front of Liberia (INPFL).
Miezi michache tu baadaye, Johnson alifanikiwa kuuteka Mji Mkuu wa Monrovia na kuuondosha udhibiti wa Taylor katika eneo hilo. Tofauti na Taylor alivyotarajia, Johnson ndiye aliyefanikiwa kumkamata Rais Doe na kumtesa hadi kifo.
Hiyo ilisababisha machafuko zaidi. Si tu kati ya Taylor na Johnson, bali pia vikaibuka vikundi vingi katika jamii, kila upande ukitaka udhibiti wa rasilimali za Liberia [chuma, dhahabu, mbao na zao la mpira].
Kwa kadiri vita vilivyoendelea baada ya utawala wa Doe kuanguka, NPFL chini ya Taylor iliweza kupata nguvu zaidi na hatimaye kudhibiti maeneo mengi nchini Liberia.
Vita vilipomalizika mwaka 1996, Liberia ilifanya Uchaguzi Mkuu wake [1997] uliosimamiwa na wapiganaji wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa na Taylor kuchaguliwa na wananchi kwa asilimia 75 ya kura.
Licha ya uchaguzi kuonekana wa huru na haki, bado wakosoaji walisema Taylor alishajiandalia mazingira ya kushinda.
Mosi, alidhibiti vyombo vingi vya habari wakati wa vita, hivyo akavitumia katika kampeni. Pili, wananchi walihofia kwamba kama angekosa urais, basi angeanzisha vita.
Yote kwa yote, Taylor alichaguliwa kuwa Rais wa Liberia kupitia Chama cha National Patriotic Party (NPP) na hiyo ikawa hatua ya kwanza ya safari yake ya kuliongoza Taifa hilo.
Utawala wake ulikosolewa vikali kwa wizi wa rasilimali, hasa dhahabu, ambapo Taylor pekee alitajwa kuvuna takribani Dola milioni 100, kiasi ambacho kwa wakati huo kilikuwa nusu ya mapato ya Serikali.
Pia, alikosolewa kwa matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu ndani ya Liberia, ikiwa ni pamoja na kuagiza vyombo vya dola, hasa jeshi, kuwashughulikia waandishi wa habari, wanasiasa wa upinzani na wanaharakati.
Mathalan, mwaka 1998, Serikali ya Taylor ilifanya jaribio la kumuua aliyekuwa mwanasiasa wa upinzani. Roosevelt Johnson [kiongozi wa zamani wa wapiganaji wa ULIMO].
Hii iliibua machafuko mjini Monrovia na ilichangia Liberia kuingia tena kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1999.
Nje ya nchi, Taylor alitanua mbawa zake za udikteta kwa kuingilia vita vya wenyewe kwa wenyewe katika nchi jirani ya Sierra Leone, ambapo Serikali yake iliunga mkono waasi wa Revolutionary United Front (RUF) kwa kuwapatia wapiganaji, fedha na silaha kuanzia mwaka 1991 hadi 2002.
Mwaka 2003, Taylor akiwa amepoteza udhibiti wa maeneo mengi kutokana na presha kutoka katika makundi ya Liberians United for Reconciliation and Democracy (LURD) na Movement for Democracy in Liberia (MODEL), wakati huo pia akiwa na mashitaka ya uhalifu wa kivita, aliamua kuiuzulu na kukimbilia Nigeria.
Miaka mitatu baadaye, Rais mpya wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf, aliziomba mamlaka za Nigeria kumkamata na kumrudisha ili kujibu mashitaka yake ya uhalifu dhidi ya binadamu.
Hatimaye, Taylor aliangukiwa na rungu la hukumu ya kifungo cha miaka 50 gerezani mwaka 2012 kwa makosa saba, yakiwamo ya ugaidi, mauaji na ubakaji wakati wa vita vya Sierra Leone.
Taylor ni mume wa mwanasiasa maarufu wa Liberia, Jewel Taylor, ambaye kwa sasa anakabiliwa na mashitaka ya utakatishaji fedha nchini Liberia. Jewel aliyeolewa na Taylor mwaka 1997, alikuwa Makamu wa Rais wakati wa utawala wa Rais George Weah [2018 – 2024].
Wakiwa wamebahatika mtoto mmoja wa kiume, Phillip Taylor, Jewel aliomba talaka wakati Taylor alipokimbilia Nigeria [akikwepa mashitaka]. Bibiye alisema uamuzi huo umetokana na Umoja wa Mataifa [UN] kumnyima kibali cha kwenda kumtembelea.
Hata hivyo, Taylor ana watoto wangine watatu katika ndoa yake na mke wa pili aitwaye Victoria Addison. Mtoto wake wa mwisho ni Charlize aliyezaliwa Machi, 2010. Victoria amewahi kulalamikia kunyimwa ruhusa ya kumtembelea mumewe gerezani huko Uingereza.
Pia, Taylor ana mtoto mwingine wa kiume, Charles McArther Emmanuel, ambaye ni raia wa Marekani. Alimpata katika mahusiano yake akiwa chuoni. Mwaka 2008, naye alihukumiwa miaka 97 gerezani kwa kuhusika katika uhalifu wakati wa baba yake akiwa Rais nchini Liberia.
Makala haya yameandaliwa na GAZETINI kwa msaada wa vyanzo vya habari vya kimataifa.


