Na mwandishi wetu, Gazetini
UTAFITI mpya wa kimataifa umebaini kuwa kati ya wakulima na wafanyakazi wa mashambani milioni 402 hadi 433 duniani wanaathiriwa na viuatilifu hatarishi kila mwaka, huku wanawake barani Afrika wakitajwa kuwa miongoni mwa makundi yaliyo katika hatari kubwa zaidi kutokana na ushiriki wao mkubwa katika shughuli za kilimo.
Utafiti huo uliofanywa na mtandao wa kimataifa wa Pesticide Action Network (PAN) na kuchapishwa katika jarida la Frontiers in Public Health Septemba 2, 2026, umechambua takwimu za kipindi cha mwaka 2006 hadi 2023 kutoka nchi 139. Matokeo yake yanaonyesha ukubwa wa changamoto ya kiafya na kimazingira inayotokana na matumizi ya viuatilifu katika uzalishaji wa chakula duniani.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa AGENDA for Environment and Responsible Development, Dorah Swai, amesema wanawake barani Afrika wako katika hatari kubwa kutokana na kushiriki kwa kiasi kikubwa katika shughuli mbalimbali za kilimo, ikiwemo kupalilia na kuvuna. Amesema ukosefu wa vifaa vya kujikinga, mafunzo duni kuhusu usalama wa viuatilifu na hali ya joto inayowafanya wakulima kutopenda kuvaa vifaa hivyo ni miongoni mwa sababu zinazoongeza hatari.
“Utafiti unaonyesha kuwa idadi ya wakulima duniani inakadiriwa kufikia milioni 934, ikimaanisha kuwa asilimia 46 ya wakulima hao huathirika na viuatilifu hatarishi kila mwaka. Idadi kubwa zaidi ya waathirika inakadiriwa kuwepo Asia Kusini, ikifuatiwa na Asia ya Kusini-Mashariki na Afrika Mashariki,” amesema Swai.
Ameongeza kuwa ukubwa wa tatizo unaweza kuwa mkubwa zaidi kwa kuwa takwimu hizo hazijumuishi watoto milioni 84 wanaofanya kazi katika sekta ya kilimo duniani, wala familia za vijijini zinazoweza kuathiriwa na viuatilifu vinavyosambaa kupitia upepo wakati wa shughuli za unyunyiziaji mashambani.
Kwa upande wake, Afisa Programu Mkuu wa AGENDA, Silvan Mng’anya, amesema athari za viuatilifu zinaweza kujitokeza kwa haraka au baada ya mtu kuendelea kuathirika kwa muda mrefu. Amesema sumu ya viuatilifu inayotokea kwa ghafla, inayojulikana kama Acute Pesticide Poisoning, inaweza kujitokeza ndani ya saa 48 baada ya mtu kuathirika.
Kwa mujibu wa Mng’anya, dalili zake zinaweza kujumuisha maumivu ya kichwa, kichefuchefu, kutapika na muwasho wa ngozi. Hata hivyo, amesema kuathirika mara kwa mara kwa muda mrefu kunaweza kuongeza hatari ya madhara makubwa zaidi kiafya, yakiwemo saratani, ulemavu wa viungo na kifo.
Utafiti huo umebaini matukio 369,632 ya kuathirika bila kukusudia kwa viuatilifu katika nchi zilizohusishwa, ambapo watu 9,182 waliripotiwa kupoteza maisha. Kwa kuzingatia takwimu hizo, watafiti wanakadiria kuwa takribani watu 11,000 hufariki duniani kila mwaka kutokana na madhara ya viuatilifu hatarishi.
AGENDA imezitaka mamlaka na wadau wa sekta ya kilimo kuchukua hatua za haraka kupunguza na hatimaye kuondoa matumizi ya viuatilifu hatarishi zaidi, huku ikihimiza matumizi ya njia mbadala salama zinazolinda afya za wakulima, watumiaji wa chakula na mazingira.
Shirika hilo pia limetaka utekelezaji wa Lengo A7 la Mwongozo wa Kimataifa wa Kemikali (GFC), linalolenga kuondoa matumizi ya viuatilifu hatarishi zaidi (Highly Hazardous Pesticides—HHPs) ifikapo mwaka 2035. Kwa mtazamo wa mazingira, hatua hiyo inalenga kupunguza madhara ya kemikali hizo kwa afya za binadamu, udongo, maji na mifumo ya ikolojia inayotegemeza uzalishaji wa chakula.


