TEHRAN, Iran
SIKU chache tu baada ya Marekani kutangaza vikwazo vipya kwa Iran, uhaba wa mafuta umeripotiwa kuyakabili maeneo mengi ndani ya nchi hiyo ya Kiarabu.
Hilo limethibitishwa na foleni kubwa katika vituo vya mafuta katika mitaa nchini humo. Katika video zilizosambaa mitandaoni, baadhi ya raia wameonakana wakiwa wamelala kwenye magari yao wakati wakisubiri zamu yao ya kujaziwa mafuta.
Katika baadhi ya maeneo, vituo vya mafuta vimefungwa kabla ya kumaliza kuhudumia na hiyo imetafsiriwa kuwa ni kuishiwa na mafuta.
Kwa mujibu wa taarifa, uhaba ni mkubwa zaidi kwa upande wa dizeli, ambapo baadhi ya madereva wa malori wanalazimika kulala kwenye vituo vya mafuta ili kupata huduma.
Taarifa pia zinaeleza kuwa kwa sasa Iran ina upungufu wa lita milioni 15 ya mafuta kwa siku, hiyo ikitokana na vita vinavyoendelea kati yake na Marekani na Israel.
Hali hiyo imetokana na uharibifu wa miundombinu uliotokana na mashambulizi ya maadui zao hao, achilia mbali hatua ya Marekani kuzuia kuingia na kutoka kwa mafuta nchini Iran.
Mmoja ya wakazi wa Karaj, Mji ulioko Magharibi mwa Tehran, amesema baadhi ya vituo vya kujaza mafuta vimeweka utaratibu wa kutokuzidisha lita tano kwa mteja mmoja.
“Niko kwenye foleni. Naweza kutumia dakika 45 kusogea hapa nilipo. Jana nilikwenda kwenye vituo vingine. Baadhi vimefungwa, vingine havikuwa na mafuta na vingine vilikuwa na foleni kubwa zaidi,” anasema.
Mwananchi mwingine, ambaye ni dereva wa malori, amesema: “Siku nzima inaishia kama si kwenye foleni, basi barabarani.”
Hata hivyo, wapo wanaoamini kuwa Serikali ya Iran imetengeneza kwa makusudi uhaba huo wa mafuta kwa lengo la kuwaandaa kisaikolojia wananchi, kabla ya kuwapandishia bei ya nishati hiyo.


